May 15, 2019 11:18 UTC
  • Baraza la Kijeshi la Sudan na wapinzani wafikia mapatano ya  kuunda serikali ya mpito

Hatimaye baada ya mazungumzo mapana na ya vuta nikuvute Baraza la Kjeshi la Mpito la Sudan na wawakilishi wa upinzani nchini humo wamefikia mapatano kuhusu muda wa miaka mitatu wa kukabidhi madaraka nchini humo na namna serikali hiyo ya muda itakavyoundwa nchini humo.

Mazungumzo yameanza huko Sudan ambapo masuala makuu yaliyokuwa yakiibua hitilafu katika duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya wapinzani na Baraza la Kijeshi la Mpito la nchi hiyo yalikuwa ni kuhusu namna serikali itakavyoundwa katika kipindi cha mpito na shaksia gani watakaojumuishwa katika baraza hilo la mpito. Hivi sasa inaonekana kuwa katika duru hii ya mazungumzo kumefikiwa mapatano kadhaa kuhusu suala hilo, hata hivyo mazungumzo yangali yanaendelea kwa ajili ya kuhitimisha mapatano kati ya pande mbili hizo. 

Jenerali Yassir al Atta mjumbe wa baraza hilo la kijeshi ametangaza kuwa: Theluthi mbili ya serikali ya muda ya Sudan katika kipindi cha mpito itawajumuisha wawakilishi wa muungano wa Ukombozi na Mabadiliko; na theluthi nyingine iliyobaki itakuwa na wawakilishi wa vyama ambavyo si kutoka katika muungano huo.  

Jenerali Yasser al Atta

Ghasia zimeshtadi Sudan hivi sasa. Wapinzani wanataka kukabidhiwa haraka madaraka kwa raia na kuundwa serikali ya kidemokrasia nchini humo. Askari usalama aidha wameshadidisha hatua za ukandamizaji dhidi ya wafanya maandamano kiasi kwamba watu kadhaa waliuawa na kujeruhiwa siku kadhaa zilizopita. Katika upande mwingine, hali hii inayoendelea huko Sudan imepelekea kuongezeka machafuko na kukandamizwa wafanya maandamano. 

Hisham Abdulmutalib Ahmad Bubakar Mkuu wa Majeshi ya Sudan bila ya kumtaja jina mtu au kundi lolote amewatuhumu vibaraka wenye ushawishi kuwa wanafanya juhudi za kusambaratisha mapatano yaliyofikiwa kati ya Baraza la Kijeshi la Sudan na muungano wa Ukombozi na Mabadiliko kuhusu muundo wa serikali katika kipindi cha mpito na kusema: Kuna vibaraka wanaojipenyeza kati ya wafanya maandamano na wapangaji wake.  

Hii ni katika hali ambayo Muungano wa Ukombozi na Mabadiliko umelitaja Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan kuwa linahusika katika kuwaua wafanya maandamano huko Khartoum mji mkuu wa nchi hiyo na umetaka kuundwa kamati ya uchunguzi na kuhukumiwa wahusika wa jinai hizo. 

Wapinzani nchini Sudan wana wasiwasi na kuendelea hali ya mambo kama ile iliyokuwepo wakati wa utawala wa Omar al Bashir na pia kuchukuliwa madaraka na wafuasi pamoja na vibaraka wa utawala huo. Wapinzani wanaona kuwa uongozi wa nchi unapaswa kukabidhiwa shakhsia wapya. Aidha wapinzani bado wanahofia kuwepo wanajeshi katika safu ya uongozi wa nchi; na hivyo kuielekeza nchi hiyo katika mfumo wa kidikteta. 

Rais wa Sudan aliyepinduliwa na jeshi, Omar Hassan al Bashir

Katika upande mwingine, hali ya wasiwasi imetanda kutokana na kuendelea uingiliaji wa nchi ajinabi huko Sudan khususan uingiliaji kati wa Saudi Arabia na Imarati; na njama za nchi hizo za kuathiri mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo. Imarati na Saudi Arabia zimekuwa zikifanya kila zinaloweza ili kuathiri mwenendo wa kisiasa wa Sudan tangu kuanza wimbi la maandamano nchini humo. Kwa kadiri kwamba hivi majuzi balozi wa Saudia nchini Sudan alidai kuwa nchi yake ndiyo inayosababisha mabadiliko yanayoshuhudiwa sasa huko Sudan.  

Hata kama inaonekana kuwa tayari hatua ya kwanza imechukuliwa kufuatia kufikiwa mapatano ya mwanzo kwa ajili ya kurejesha utulivu wa kisiasa nchini humo na kuhitimisha wimbi la maandamano, lakini wapinzani na baraza la kijeshi la mpito wangali wanakabiliwa na vizuizi mbalimbali.

Tags