May 16, 2019 06:31 UTC
  • Zaidi ya nusu ya wanawake nchini Morocco wanakabiliwa na ukatili

Uchunguzi rasmi uliotangazwa nchini Morocco unaonyesha kwamba, zaidi ya nusu ya wanawake wa nchi hiyo wanakumbwa na ukatili dhidi yao.

Uchunguzi huo pia umeonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wa Morocco, hawajawashtaki watu wanaowafanyia ukatili huo. Wizara ya Familia ya Morocco ilifanya uchunguzi huo kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu kwa kuwashirikisha zaidi ya wanawake elfu 13,500 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 64. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 54 ya wanawake hao ni wahanga wa aina fulani ya ukatili dhidi yao.

Wanaharakati wa haki za wanawake nchini Morocco

Aidha imeongeza kwamba ukatili wa kisaikolojia kuwalenga wanawake unashika nafasi ya kwanza na baada yake unafuatia ukatili wa kiuchumi, kimwili na kijinsia. Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo ambayo yamesambazwa na Wizara ya Familia nchini Morocco, wanawake wenye umri wa miaka 25 hadi 29 ndio wako hatarini zaidi kukumbwa na ukatili huo. Ukatili wa kifamilia ni jambo lililoenea sana nchini Morocco ambapo asilimia 52 ya wanawake walioolewa wanapitia wakati mgumu kutokana na wimbi hilo la utumiaji mabavu dhidi yao.

Tags

Maoni