May 17, 2019 02:31 UTC
  • Wapinzani Sudan wasikitishwa na hatua ya jeshi kusimamisha mazungumzo

Wapinzani nchini Sudan wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya Baraza la Kijeshi la Mpito ya kusimamisha kwa muda mazungumzo baina ya pande mbili hizo kuhusu uundwaji wa serikali ya muda nchini humo.

Muungano wa upinzani nchini humo uliyasema hayo jana Alkhamisi na kubainisha kuwa, kusimamishwa mazungumzo hayo kwa muda wa siku tatu ni kizingiti kingine katika jitihada za kufungua ukurasa mpya wa demokrasia nchini humo.

Wapinzani nchini Sudan wanasisitiza kuwa, madhali Baraza la Mpito la Kijeshi halijakabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia, maandamano na malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo yataendelea kushuhudiwa.

Viongozi wa maandamano nchini Sudani wamekuwa wakilituhumu Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kwamba, linapoteza muda na hivyo kuchelewesha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Maandamano ya wananchi mjini Khartoum

Siku ya Jumatano, Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan lilitangaza kusimamisha mazungumzo na wapinzani likisisitiza kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa lengo la kupunguza tofauti kati ya pande mbili.

Awali baraza hilo lilitangaza kwamba limekubaliana na wapinzani hao kushikilia uongozi kwa muda wa miaka mitatu kuelekea utawala wa kiraia na kwamba ndani ya masaa 24 pande hizo zingefikia mwafaka kamili kuhusiana na suala hilo.

Tags