May 21, 2019 13:30 UTC
  • Wapinzani Sudan waitisha mgomo wa nchi nzima, wasema mazungumzo yamefeli

Viongozi wa upinzani nchini Sudan wametoa mwito wa kufanyika mgomo wa nchi nzima, wakisisitiza kuwa vikao viwili vya mazungumzo vya juzi na jana jioni vimeshindwa kupatia ufumbuzi hitilafu zilizopo baina ya pande mbili.

Bila kutaja siku ya kuanza mgomo huo, Chama cha Wanataaluma cha Sudan kimesema leo Jumanne kuwa, wananchi wa Sudan wanataka kuona jeshi likikabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia na hivyo kuwataka wafuasi wao kujiandaa kwa mgomo wa taifa zima.

Taarifa ya chama hicho imesema, "Utawala wa kiraia una maana kuwa, mfumo wa uongozi nchini unapaswa kuongozwa na raia kwa asilimia kubwa katika kila uga."

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan kwa upande wake linasisitiza kuwa, suala tata lililobaki hivi sasa ni juu ya muundo wa baraza huru la mpito linalopaswa kuongoza nchi hiyo hadi uchaguzi mkuu ufanyike, lakini limebainisha kuwa linafanya juu chini kuondoa hitilafu zilizopo.

Baadhi ya wakuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan

Hivi sasa kuna mivutano mingi baina ya wanajeshi waliofanya mapinduzi na viongozi wa wananchi kuhusu muundo wa serikali ya mpito na watu wanaopaswa kuunda serikali hiyo.

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan ambalo linaiongoza Sudan kwa sasa, liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.

Tags