May 25, 2019 07:08 UTC
  • Mgomo wa nchi nzima wa wapinzani nchini Sudan kufanyika wiki ijayo

Viongozi wa upinzani nchini Sudan wametangaza Jumanne ya wiki ijayo kuwa siku ya kuanza mgomo wa nchi nzima, baada ya mazungumzo ya kutatua hitilafu zilizopo baina yao na Baraza la Mpito la Kijeshi kushindwa kuzaa matunda.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na makundi ya upinzani na asasi zinazoongoza maandamano nchini humo imewataka wananchi wote Sudan, wawe katika sekta za umma au binafsi washiriki mgomo huo wa siku mbili wa wiki ijayo, kwa lengo la kulishinikiza jeshi likabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo.

Taarifa hiyo imesema mgomo huo utaandamana na maandamano ya nchi nzima, ambapo wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika medani za miji mikubwa ya nchi hiyo kushiriki maandamano hayo, ukiwemo mji mkuu Khartoum.

Hata hivyo wamesisitiza kuwa, wana wingi wa matumaini kwamba huenda muafaka kati yao na jeshi ukafikiwa kabla ya Jumanne hiyo.

Baraza la Mpito la Kijeshi linalotawala Sudan hivi sasa

Hivi sasa kuna mivutano mingi baina ya wanajeshi waliofanya mapinduzi na viongozi wa wananchi kuhusu muundo wa serikali ya mpito na watu wanaopaswa kuunda serikali hiyo.

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan ambalo linaiongoza Sudan kwa sasa, liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Omar Hassan al Bashir.

Tags