May 27, 2019 04:25 UTC
  • Wapinzani nchini Sudan watofautiana juu ya mgomo wa nchi nzima

Muungano mkuu wa upinzani nchini Sudan umepinga mwito wa baadhi ya makundi ya wapinzani wa kufanyika mgomo wa nchi nzima kuanzia Jumanne ijayo, baada ya mazungumzo ya kutatua hitilafu zilizopo baina yao na Baraza la Mpito la Kijeshi kushindwa kuzaa matunda.

Hayo yalisemwa jana Jumapili na chama kikuu cha upinzani cha Umma, ambacho kilikuwa mstari wa mbele katika maandamano yaliyomng'oa madarakani Omar al Bashir.

Katika taarifa, chama hicho kimesema, "Sisi Muungano wa Uhuru na Mabadiliko, ambayo ni harakati kuu ya maandamano ya wananchi wa Sudan tunapinga mgomo uliotishwa na baadhi ya makundi ya upinzani."

Chama hicho kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Sadiq al-Mahdi kimesema uamuzi kama huo unapaswa kuchukuliwa na baraza la viongozi wa maandamano ambalo linapaswa kuundwa leo Jumatatu.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa iliyopita na makundi hayo ya upinzani na asasi zinazoongoza maandamano nchini humo imewataka wananchi wote Sudan, wawe katika sekta za umma au binafsi washiriki mgomo huo wa siku mbili kuanzia Jumanne ijayo, kwa lengo la kulishinikiza jeshi likabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo. 

Maandamano ya wananchi wa Sudan

Taarifa hiyo imesema mgomo huo utaandamana na maandamano ya nchi nzima, ambapo wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika medani za miji mikubwa ya nchi hiyo kushiriki maandamano hayo, ukiwemo mji mkuu Khartoum.

Hivi sasa kuna mivutano mingi baina ya wanajeshi waliofanya mapinduzi na viongozi wa wananchi kuhusu muundo wa serikali ya mpito na watu wanaopaswa kuunda serikali hiyo.

Tags