Jun 04, 2019 13:30 UTC
  • Wapinzani nchini Sudan wapinga mpango wa jeshi wa kukabidhi madaraka

Wapinzani nchini Sudan wametangaza kuwa wanapinga mpango wa kukabidhi madaraka uliotangazwa na Baraza la Mpito la Kijeshi lililotwaa madaraka ya nchi baada ya kujiri maandamano yaliyompindua rais Omar al Bashir wa nchi hiyo mwezi Aprili mwaka huu.

Madani Abbas Madani, mkuu wa muungano mkuu wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko ambao umekuwa mstari wa mbele katika maandamano ya kulishinikiza jeshi likabidhi madaraka kwa raia, amesema maandamano na uasi wa kiraia utaendelea hadi pale Baraza la Mpito la Kijeshi litakapokabidhi madaraka kwa raia.

Amesema "yale yote yaliyofanyika yakiwemo mauaji ya umati dhidi ya waandamanaji, kuwajeruhi na kuwadhalilisha yamefanyika kwa mpangilio maalumu kwa shabaha ya kukandamiza matakwa ya wananchi wa Sudan."

Wapinzani wametangaza msimamo huo masaa machache baada ya jeshi la Sudan kuvunja makubaliano yote ya kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia na badala yake likatangaza uchaguzi mkuu katika kipindi cha miezi tisa ijayo. Hayo yamekuja baada ya wanajeshi kushambulia waandamanaji na kuua raia zaidi ya 30 na kujeruhi mamia ya wengine jana Jumatatu.

Baadhi ya wakuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi 

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kitendo cha askari usalama wa Sudan cha kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia.

Msemaji wa Guterres, Stephane Dujarric amesema, Katibu Mkuu wa UN anafuatilia mashambulizi ya askari hao yaliyosababisha vifo na majeruhi ya watu wengi na kueleza wasiwasi wake  kuhusu ripoti za askari hao kufyatua risasi ndani ya vituo vya afya.

Kadhalika taasisi nyingine za kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya zimelaani mauaji ya raia nchini Sudan. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo Jumanne kujadili hali inayoendelea kushuhudiwa nchini Sudan.

Tags