Jun 11, 2019 08:19 UTC
  • Wapinzani Sudan kuwateua watu 8 kuongoza Baraza la Mpito

Makundi ya upinzani yanayoongoza maandamano na uasi wa kiraia nchini Sudan yanapanga kuteua watu wanane katika Baraza la Mpito, huku yakimteua mchumi mashuhuri nchini kuwa kiongozi wa serikali hiyo ya muda.

Muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko umetangaza kumteua Abdullah Hamdouk, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika kuwa Waziri Mkuu wa serikali ijayo ya mpito. Aidha muungano huo umewateua wanawake watatu kuwa wanachama wa baraza hilo.

Tangazo hilo limetolewa ikiwa leo ni siku ya tatu ya kampeni ya uasi wa kiraia wa nchi nzima iliyoanza siku ya Jumapili nchini Sudan. Kwa akali watu wanne waliripotiwa kuuawa na maafisa usalama katika siku ya kwanza ya kampeni hiyo.

Kadhalika kampeni hiyo ya uasi wa kiraia imepelekea mji wa Khartoum na miji mingine mikubwa ya nchi kusalia mahame, huku maduka na vituo vingi vya biashara vikifungwa.

Baraza la Mpito la Kijeshi Sudan linalotuhumia kuua makumi ya waandamanaji hivi karibuni

Hii ni katika hali ambayo, Shamsuddin al Kabbashi, Msemaji wa Baraza la Kijeshi la Serikali ya Mpito ya Sudan ametangaza kuwa baraza hilo liko tayari kufanya mazungumzo bila ya masharti na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa nchi hiyo, kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Hata hivyo Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa Sudan umesema kuwa ili kuendelea kufanya mazungumzo na Baraza la Kijeshi kuna udharura wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kuchunguza mauaji ya makumi ya watu wakati askari usalama walipowavamia wapinzani waliokuwa katika mgomo wa kuketi chini mjini Khartoum. 

Tags