Jun 24, 2019 06:33 UTC
  • Wamorocco waandamana kupinga mkutano wa Bahrain wa kuangamiza kadhia ya Palestina

Maelfu ya wananchi wa Morocco wamefanya maandamano makubwa kupinga mkutano wa kufungua mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne wa kuangamiza kadhia ya Palestina uliopangwa kufanyika kesho na keshokutwa Jumatano katika mji mkuu wa Bahrain, Manama.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa maelfu ya wananchi wa Morocco walifanya maandamano jana mjini Rabat wakiwa na bendera za Palestina kutangaza upinzani wao mkali kwa mkutano huo wa Manama. Waandamanaji hao wamelaani mpango wa Marekani wa Muamala wa karne na kuzishutumu nchi za Kiarabu zinazopigania mpango huo hasa Saudi Arabia kwa kulisatili taifa la Palestina.

Waandamanaji hao wamechoma moto pia bendera za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuitaka serikali ya Morocco itangaze rasmi upinzani wake kwa mpango huo wa Marekani. Huku hayo yakiripotiwa, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina naye amepinga vikali mkutano huo wa Manama na kusema kuwa, mpango wa Marekani wa kuangamiza kadhia ya Palestina utafeli tu. 

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina

 

Akizungumza na maafisa wa chama chake cha Fat'h huko Ramallah siku ya Jumamosi, Mahmoud Abbas kwa mara nyingine alipinga vikali mpango huo wa Marekani na kusisitiza kuwa, matatizo ya kiuchumi hayawezi kutatuliwa kabla ya kupatikana kwanza usalama na suluhisho la kisiasa.

Rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza kuwa mkutano wa Manama ni wa kuisaliti kadhia ya Palestina na kwamba mpango huo umefeli hata kabla ya kuanza utekelezaji wake. Itakumbukwa kuwa hakuna Mpalestina yoyote anayeunga mkono mpango huo wa Marekani kutokana na kudharau kwake masuala yote ya dharura kwa Wapalestina. 

Tags

Maoni