Jul 17, 2019 07:32 UTC
  • Wapinzani Sudan: Wanajeshi wasipewe kinga ya kushtakiwa

Muungano mkuu wa upinzani nchini Sudan umepinga vikali mpango wa kuwapa wanajeshi wa nchi hiyo kinga mutlaki ya kushtakiwa, ukisisitiza kuwa waliohusika na vitendo vya jinai wanapaswa kubebeshwa dhima.

Ismail al-Taj, kiongozi wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Sudan (SPA) ambayo ni sehemu ya muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko amesema kadhia hiyo ya kutofikishwa mahakamani wanajeshi ni katika mambo yaliyochelewesha kusainiwa makubaliano ya kisiasa baina ya wapinzani na wanajeshi.

Wawakilishi wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko wamesaini hii leo hati ya makubaliano ya kisiasa, shughuli ambayo ilitazamiwa kufanyika Jumamosi iliyopita, saa chache baada ya jeshi hilo kudai kuwa limezima jaribio la mapinduzi, lakini ikaakhirishwa.

Usiku wa kuamkia jana, kundi kubwa la wananchi wa Sudan lilimiminika katika barabara za wilaya moja ya Khartoum kulalamikia kuuliwa raia mmoja na wanajeshi wa nchi hiyo.

Itakumbukuwa kuwa, hivi karibuni wawakilishi wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko walifikia makubaliano ya kugawana madaraka ya nchi. Aidha pande mbili zilikubaliana kuunda jopo huru litakalochunguza vitendo vya ghasia na mauaji ya hivi karibuni.

Maandamano ya usiku wa kuamkia jana mjini Khartoum

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Baraza la Kijeshi la Mpito lilikabiliana kwa mkono wa chuma na maandamano ya wananchi, ambapo watu 11 waliuawa na wengine zaidi ya 180 kujeruhiwa. 

Aidha Juni 3, watu wengine 125 waliuawa katika wimbi jipya la utumiaji nguvu kupita kisiasa wa maafisa usalama wa Sudan dhidi ya waandamanaji waliotaka kukabidhiwa madaraka kwa raia mjini Khartoum.

Tags