Jul 25, 2019 02:40 UTC
  • Rais wa zamani wa Gambia atuhumiwa kufanya mauaji dhidi ya wahajiri

Rais wa zamani wa Gambia ametuhumiwa kwamba mwaka 2005 alitoa amri ya kutekelezwa mauaji ya umati dhidi ya wahajiri 30 pamoja na mwandishi mmoja wa habari.

Hayo yamesemwa na Omar Jalo mmoja wa watu waliohusika na mauaji hayo na ambaye pia ni mmoja wa askari wa zamani wa gadi ya rais huyo wa zamani wa Gambia wakati wa kutoa ushahidi katika kesi inayohusiana na mauaji hayo. Kwa mujibu wa Jalo, mwaka 2005 Yahya Jammeh, rais wa zamani wa Gambia, alitoa amri ya kuuawa wahajiri 30 akiwemo pia mwandishi mmoja wa habari raia wa Ufaransa. Hii ni katika hali ambayo Jammeh alidai kwamba wahajiri hao 30 ni vibaraka ambao walikuwa wanakusudia kuuondoa madarakani utawala wake.

Wahajiri wa Kiafrika ambao huyatia hatarini maisha yao kwa lengo la kutafuta maisha mazuri barani Ulaya

Askari huyo wa timu iliyohusika kufanya mauaji ametoa ushahidi huo ambapo siku moja kabla, askari mwingine wa jeshi la Gambia alinukuliwa akisema kuwa Yahya Jammeh alitoa amri ya kuuawa mwandishi wa habari wa Ufaransa aliyeandika makala iliyokosoa ufisadi na dhulma za rais huyo wa zamani wa nchi hiyo. Aidha katika ushahidi Omar Jalo amesema kuwa mwaka 2005, jeshi la Gambia liliwatia mbaroni karibu wahajiri haramu 45 kutoka Ghana, Nigeria, Senegal na Togo ambao walikuwa wanaelekea Ulaya katika pwani ya nchi hiyo na kwamba baada ya hapo Jammeh alitoa amri ya kuuawa watu hao. Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Right Watch limetoa ripoti likisema kwamba, wahajiri wengine 15 hawajulikani waliko na kwamba kuna uwezekano nao pia waliuawa kwa amri ya rais huyo wa zamani wa Gambia. Gambia ni moja ya makoloni ya zamani ya Uingereza ambayo ilianza kutawaliwa na Yahya Jammeh mwaka 1994 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyotekelezwa kupitia umwagaji damu.

 

Tags

Maoni