Jul 31, 2019 01:18 UTC
  • Mfalme wa Morocco ashikilia msimamo wa kuipa Sahara Magharibi mamlaka yake ya ndani tu

Mfalme Mohammed VI wa Morocco amesema, kutoa mamlaka ya ndani kwa Sahara Magharibi ya kujiendeshea mambo yake ndiyo njia pekee ya kutatua mgogoro wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la Al-Qudsul-Araby, Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco ameshikilia msimamo wa serikali yake wa kulipatia eneo la Sahara Magharibi mamlaka ya kujiendeshea mambo yake, lakini likibaki kuwa chini ya mamlaka ya serikali kuu ya Rabat na kueleza kwamba, kufanya hivyo ndiyo njia pekee ya kuupatia utatuzi mzozo wa eneo hilo.

Mfalme wa Morocco amesisitiza kuwa: Sahara Magharibi itabaki kuwa ndani ya mipaka ya ardhi ya Morocco.

Sahara Magharibi ni eneo lililoko kaskazini magharibi mwa Afrika na kusini mwa nchi ya Morocco, ambapo pande mbili za serikali ya Rabat na Harakati ya Ukombozi ya Polisario zinazozania udhibiti wa eneo hilo.

Mwaka 1976, harakati ya Polisario ilitangaza habari ya kuundwa nchi iitwayo "Jamhuri ya Sahara", mji mkuu wake ukiwa ni Al-Ayuun, uamuzi ambapo ulipingwa na Morocco na kuzusha mapigano katika eneo hilo.

Harakati ya Ukombozi ya Polisario inataka iitishwe kura ya maoni itakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuamua hatima ya kuwa au kutokuwa huru na kujitawala eneo la Sahara Magharibi.../

Tags

Maoni