Sep 03, 2019 13:28 UTC
  • Liberia yatangaza hali ya hatari kutokana na wimbi la homa ya Lassa

Vyombo vya mamlaka ya masuala ya afya nchini Liiberia vimetangaza hali ya hatari kutokana na mfumuko wa homa ya Lassa ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu wasiopungua 21 nchini humo katika mwaka huu wa 2019.

Afisa mkuu wa masuala ya tiba wa Liberia, Francis Kateh amewaambia waandishi wa habari kwamba, kaunti nne zimeathiriwa sana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya homa hiyo ya Lassa.

Ameongeza kuwa jambo linalotia wasiwasi zaidi ni kwamba, homa hiyo ya Lassa imewapata wafanyakazi wa sekta ya afya waliopewa mafunzo ya kupima na kushughulikia watu waliopatwa na ugonjwa huo

Francis Kateh amesema kuwa, mtaalamu wa maabara pia amegunduliwa kuwa miongoni mwa watu waliofariki dunia kutokana na homa hiyo hatari katika kipindi cha kati ya Januari Mosi na Agosti 25.

Homa hiyo ya Lassa tayari imeyakumba maeneo na kaunti za Nimba, Grand Bassa, Bong na Grand Kru.

Ugonjwa wa homa ya Lassa ulishuhudiwa kwa mara ya kwanza nchini Nigeria mwaka 1969 katika mji wa Lasa na kwa sababu hiyo ulipewa jina la mji huo. Ugonjwa huo unashabihiana sana na ule wa Ebola na Marbug.

Mwaka jana ugonjwa huo uliua zaidi ya watu 140 nchini Nigeria katika kipindi cha baina ya Januari na Aprili.

Dalili za ugonjwa huo ambao hukaa mwilini kati ya siku 6 na 21 ni mtu kujisikia mnyonge, baada ya siku chache mgonjwa huanza kuumwa na kichwa, kuwashwa na koo, kuumwa kifua, kutapika, kuharisha, na kusokotwa na tumbo. Vilevile uso wa mgonjwa  unaweza kufura, kuumwa na mapafu na kutokwa damu mdomoni.   

Tags