Sep 05, 2019 12:17 UTC
  • Morocco yazima njama na hujuma ya kigaidi ya Daesh

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imetangaza kuwa imezima mpango wa kundi la kigaidi la Daesh nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imesema kuwa, askari wa Idara ya Ulinzi wa Taifa leo Alkhamisi wamegundua na kusambaratisha genge la wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh lililokuwa na njama ya kushambulia maeneo nyeti nchini humo. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, genge hilo lililokuwa na wanachama watano lilikuwa likiendesha shughuli zake katika miji miwili Berkane na Nador na limekamatwa na zana kadhaa za kieletroniki na silaha baridi. 

Taarifa za awali zinaonesha kuwa, wanachama wa kundi hilo la wanachama wa Daesh walikuwa na nia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya vituo na taasisi muhimu nchini Morocco. 

Nchi za kaskazini mwa Afrika zikiwemo Morocco na Algeria zimeanzisha kampeni kubwa ya kupambana na makundi ya kigaidi hususan lile la Daesh. 

Baada ya kupata kipigo cha mbwa katika nchi za Iraq na Syria, mabaki ya wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wamekimbilia katika baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu hususan katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika. 

Tags

Maoni