Sep 11, 2019 11:13 UTC
  • Kuendelea uadui dhidi ya Waislamu wa Nigeria; 12 wauawa shahidi katika kumbukumbu ya Ashura

Ikiwa ni katika kuendeleza siasa za chuki na uadui za serikali ya Nigeria dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo, vikosi vya usalama jana viliwafyatulia risasi Waislamu walioshiriki katika kumbukkumbu ya Ashura na kuwaua shahidi kwa akali waombolezaji 12 na kuwajeruhi makumi ya wengine.

Hii si mara ya kwanza kwa wanajeshi wa Nigeria kuwashambulia waombolezaji wa kumbukumbu ya  kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW Imam Hussein AS katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Mwaka 2015 vyombo vya usalama vya Nigeria viliwashambulia Waislamu katika mji wa Zaria waliokuwa katika maombolezo ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS na kuwaua na kuwajeruhi mamia miongoni mwao. Aidha Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na mkewe watiwa mbaroni.

Licha ya kutiwa mbaroni Sheikh Zakzaky na kuongezeka mashinikizo ya vyombo vya usalama  vya Nigeria dhidi ya mikusanyiko ya kidini ya Waislamu wa nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni, lakini Waislamu hao wangali wanahudhuria kwa nguvu zao zote si tu katika marasimu na mikusanyiko ya kidini, bali hata katika maandamano na mikusanyiko ya kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky. Mashinikizo ya Waislamu hao yaliilazimisha serikali ya Nigeria mwezi uliopita itoe idhini ya kuwnda kutibiwa nchini India Sheikh Ibrahim Zakzaky, ingawa mwanazuoni huyo hakutibiwa kwani alilazimika kurejea Nigeria kutokana na njama na ukwamishaji mambo wa serikali ya India kwa ushirikiano na serikali ya Abuja katika mwenendo mzima wa matibabu ya mwanazuoni huyo.

Kumbukumbu ya Ashura nchini Nigeria

Kwa hakika serikali ya Nigeria imeongeza mashinikizo dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo  kwa sababu kuu mbili. Mosi, viongozi wa Nigeria hawafurahishwi hata kidogo na sera za kupigania uadilifu na uhuru za viongozi wa Kiislamu hususan Sheikh Zakzaky zinazolenga kuleta mwamko miongoni mwa Waislamu wa kukabiliana na dhulma na ukandamizaji sambamba na ukosoaji wa kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria dhidi ya sera za Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo. Viongozi wa Nigeria wanahisi kwamba, kuongezeka mwamko miongoni mwa jamii ya Kiislamu ni hatari na tishio kwao.

Valeria Rodriguez, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Muhamadu Buhari dhidi ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na harakati nyingine za upinzani za nchi hiyo chimbuko lake ni  kuwa, serikali ya Nigeria ni serikali kidikteta na kwa muktadha huo imekuwa ikifanya njama za kuitokomeza harakati hiyo ya Kiislamu na kuzima kabisa sauti yake

Jambo la pili ni uhusiano wa karibu uliopo baina ya baadhi ya viongozi wa serikali na wa usalama wa Nigeria na Marekani, Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel na kutekelezwa siasa zilizo dhidi ya Uislamu na kuwakandamiza Waislamu katika fremu ya maslahi yao. Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, baadhi ya makamanda wa polisi na jeshi na hata baadhi ya mawaziri wamekuwa wakipokea fedha kutoka Saudia huku baadhi ya maafisa wa jeshi wakipata mafunzo huko Israel.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria

Dahiru Yahya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bayero nchini Nigeria anasema: Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni zinashirikiana kwa karibu na serikali ya Nigeria. Udhamini wa kifedha na kiidiolojia umekabidhiwa Saudia huku utawala wa Israel ukipewa jukumu la kupanga mikakati, mauaji na kupora mali za Mashia wa Nigeria. Maudhui hii ya Wazayuni na Mawahabi kushirikiana dhidi ya Waislamu iko wazi na wala suala hilo halina shaka yoyote.

Licha ya kuwa viongozi wa Nigeria walikuwa na matumaini kwamba, kwa kufanya ukandamizaji na kushadidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo, wangeweza kuwafanya Waislamu hao wasalimu amri na kuachana na harakati zao kama ambavyo wangeacha kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini kuendelea kusimama kidete Waislamu hao na kusisitiza kufanya shughuli na marasimu ya kidini ikiwemo kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS katika mwezi wa Muharram, ni mambo ambayo yamewafanya viongozi wa Abuja watangulize mbele vitendo na ukandamizaji na mauaji dhidi ya Waislamu.

Massoud Shadjareh, Mkuu wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) yenye makao yake makuu mjini London, Uingereza anasema: Serikali ya Nigeria inatumia kila mbinu kumuua Sheikh Zakzaky na kuangamiza harakati yake ya Kiislamu ili kuandaa uwanja wa kurejea ubeberu wa Magharibi barani Afrika. Hata hivyo inaonekana kuwa, licha ya mashinikizo na njama zote hizo za viongozi wa serikali ya Nigeria, lakini Waislamu wa nchi hiyo kutokana na kusoma na kufahamu alama za nyakati, wangali wanaendelea na siasa zao za kusimama kidete na kufanya juhudi za kupigania uhuru.

Tags

Maoni