Sep 12, 2019 04:05 UTC
  • Mazungumzo ya kitaifa Cameroon kuhusu eneo linalotaka kujitenga

Rais Paul Biya wa Cameroon ametoa mwito wa kuwepo kwa mazungumzo na mjadala wa kitaifa ili kutatua matatizo ya nchi hiyo ukiwemo mgogoro katika majimbo mawili ya nchi hiyo yanayotumia lugha ya Kiingereza ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi na ambayo yanataka kujitenga na kujitangazia uhuru.

Mazungumzo hayo yanapangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, na yatalenga kukidhi matarajio ya watu wa majimbo hayo. Waziri Mkuu wa Cameroon Joseph Dion Ngute ataendesha mkutano huo utakaowakutanisha maafisa wa serikali na wawakilishi wa makundi ya wanaotaka kujitenga.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha wito wa Rais Biya, na kuhimiza serikali ya Cameroon kuhakikisha kuwa mchakato wa majadiliano unakuwa shirikishi na unashughulikia changamoto zinazoikabili nchi.

Akizungumza Jumanne usiku, Rais Biya ametoa wito kwa wapiganaji wa makundi yanayotaka kujitenga katika maeneo yanayozungumza Kiingereza kujisalimisha ili kupata msamaha la sivyo hatua za kijeshi zitachukuliwe dhidi yao.

Pia ambaye amekuwa akitawala Cameroon tokea mwaka 1982, amesema amechukua hatua kadhaa kujaribu kutatua mgogoro wa maeneo yanayotaka kujitenga. Aidha amekanusha madai kuwa maeneo yanayozungumza Kiingereza yanabaguliwa katika nchi hiyo ambayo lugha yake rasmi ni Kifaransa. Amesema amewateua mawaziri kutoka maeneo hayo.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, tokea, mwaka 2017, karibu watu 1,700 wameuawa katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza nchini Cameroon na wengine 530,000 kukimbia makazi yao huku milioni 1.3 wakihitaji misaada.

Maoni