Sep 17, 2019 12:21 UTC
  • Mgombea urais nchini Tunisia apinga uhusiano wa aina yoyote na Israel

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Tunisia, wameeneza video ya mgombea urais katika uchaguzi wa sasa nchini humo ambaye ameelezea kupinga kuboreshwa uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika video hiyo, Kaïs Saïed amenukuliwa akisema: "Sisi hivi sasa tuko vitani na utawala wa Kizayuni, na kuboresha uhusiano na utawala huo ni hiyana kubwa." Kadhalika mgombea huyo wa urais nchini Tunisia ameongeza kwamba kuboreshwa uhusiano na Israel si tu kwamba ni jinai, bali ni hiyana kubwa kwa Tunisia. Kaïs Saïed amezidi kufafanua kuwa, mtu yeyote anayeamiliana na adui Mzayuni, ni haini na hiyana yake ni kubwa ambayo inapasa kuwajibishwa, na hata kama mahkama za leo zisipomshughulikia, basi atawajibishwa na wananchi.

Kaïs Saïed, mgombea urais nchini Tunisia

Aidha akizidi kubainisha kuwa hii leo Tunisia iko vitani na utawala wa Kizayuni, mgombea huyo wa urais amesema kuwa utawala huo umewafanya raia wa Palestina kuwa wakimbizi na hivi sasa pia unaendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Uchaguzi wa rais nchini Tunisia ulifanyika siku ya Jumapili iliyopita, ambapo Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo imemtangaza Kaïs Saïed na Nabil Karoui kuingia katika duru ya pili kutokana na kushindwa kupata asilimia inayohitajika ya ushindi wa moja kwa moja kwenye uchaguzi.

Tags

Maoni