Sep 18, 2019 13:31 UTC
  • Misri yataka mpatanishi katika mgogoro wake na Ethiopia kuhusu bwawa

Misri imesema inakaribisha upatanishi au uingiliaji kutoka chombo chochote kile ambacho kitasaidia kulinda na kufikia maslahi ya nchi zilizoko kwenye Mto Nile kuhusu bwawa kubwa linalojengwa na Ethiopia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenzake wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian wakiwa mjini Cairo.

Ameongeza kuwa wanajaribu kuonesha kuwa kuna nia thabiti ya kushughulikia suala hilo lenye utata la ujenzi wa bwawa la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD). Shoukry amesema wanataka kuhakikisha maslahi ya nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia yatalindwa katika muafaka utakaofikiwa.

Misri inasema kuwa, ujenzi wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance juu ya maji ya Mto Nile utapunguza hadi nusu sehemu ya maji yake katika mto huo, madai ambayo yanakanushwa na serikali ya Addis Ababa.

Sameh Shoukry

Mradi huo wa Ethiopia unaungwa mkono pia na Sudan ambapo nchi hizo mbili zinasema kuwa, kila nchi ina haki ya kutumia vizuri rasilimali zake kujiletea maendeleo.

Itakumbukwa kuwa, maji ya Mto Nile ndio mshipa wa uhai kwa Misri kwa karne nyingi na mara zote Cairo imekuwa ikiichukulia kwa hisia kali kila hatua ya kutumia maji ya Mto Nile ambayo inaweza kupunguza kiwango cha maji ya mto huo yanayofika nchini Misri.

Maoni