Sep 30, 2019 07:33 UTC
  • Rais wa Senegal atangaza msamaha kwa kinara wa upinzani

Rais Macky Sall wa Senegal ametangaza msahama kwa kiongozi wa upinzani nchini humo, Khalifa Sall ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano jela tokea mwaka jana 2018 baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya ufisadi iliyokuwa ikimkabili.

Meya huyo wa zamani wa Dakar ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa serikali ya Rais Macky Sall, kabla ya hukumu hiyo alikuwa akishikiliwa korokoroni kwa miezi kadhaa kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma na kugushi vyeti.

Mwanasiasa huyo wa upinzani amekuwa kizuizini kwa madai kuwa aliiba Franca bilioni 1.8 za nchi hiyo, sawa na zaidi ya dola milioni 3.3 za Marekani, ingawaje binafsi amekuwa akipinga madai hayo, akisisitiza kuwa kitendo hicho ni hujuma ya kisiasa.

Itakumbukwa kuwa, katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Julai mwaka juzi, muungano wa upinzani unaoongozwa na Khalifa Sall ulishika nafasi ya pili ukifuatiwa na muungano ulioundwa na Abdoulaye Wade, Rais wa zamani wa Senegal.  

Rais Macky Sall wa Senegal 

Rais Macky Sall wa Senegal alishinda tena kiti cha urais kwa kuibuka na ushindi wa asilimia 58 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika Februari mwaka huu.

Hata hivyo kambi ya upinzani ilitoa tangazo ikieleza kuwa, duru ya pili ya uchaguzi huo haiepukiki kutokana na kuwa, hakuna mgombea yeyote aliyepata asimilia 50 ya kura.

Wadadisi wa mambo wanasema meya huyo wa zamani wa Dakar angetoa ushindani mkali kwa Rais Sall iwapo angegombea urais katika uchaguzi uliopita.

Tags