Oct 20, 2019 07:27 UTC
  • Upinzani Msumbiji wakataa kukubali matokeo ya uchaguzi

Chama kikuu cha upinzani cha Renamo nchini Msumbiji kimepinga matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne iliyopita.

Viongozi wa chama hicho wametoa mwito wa kubatilishwa matokeo ya uchaguzi huo, wakisisitiza kuwa serikali imekiuka makubaliano ya amani kwa kutumia vitisho na ghasia katika siku ya uchaguzi. Wanasisitiza kuwa uchaguzi huo umezungukwa na mizengwe na uchakachuaji wa matokeo.

Matokeo ya muda yalitolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE) yanaonesha kuwa, Rais Filipe Nyusi na chama chake cha Frelimo wanaelekea kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa rais na Bunge.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Nyusi anaongoza kwa asilimia 69 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa, huku kinara wa chama cha upinzani cha Renamo, Ossufo Momade akiambulia asilimia 25 ya kura hizo.

Rais Filipe Nyusi baada ya kupiga kura. Anatazamiwa kuhifadhi kiti chake

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yanapaswa kutolewa ndani ya siku 15 baada ya kufanyika uchaguzi. Haijabainika ni asilimia ngapi ya Wamsumbiji milioni 13 waliosajiliwa kama wapiga kura walishiriki zoezi hilo la Jumanne iliyopita.

Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2014, Nyusi aliibuka mshindi katika uchaguzi wa urais kwa kuzoa asilimia 57 ya kura, huku Afonso Dhlakama, mtangulizi wa Momade wa chama cha upinzani cha Renamo akipata asilimia 37 ya kura.

Tags