Oct 23, 2019 02:46 UTC
  • Abiy Ahmed: Tukilazimika tutaingia vitani na Misri kwa ajili ya bwawa la El Nahdha

Waziri Mkuu wa Ethiopia ametahadharisha kuwa, nchi hiyo itakusanya mamilioni ya wapiganaji iwapo italazimika kingia vitani na Misri katika mzozo wa ujenzi wa bwawa la El Nahdha juu ya maji ya Mto Nile.

Abiy Ahmed ameyasema hayo katika Bunge la Ethiopia lililojadili masuala kadhaa muhimu ikiwemo kadhia ya bwawa la El Nahdha na kusisitiza kuwa, mazungumzo yanaweza kutatua mzozo huo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia ameongeza kuwa, nchi yake imeazimia kukamilisha mradi wa huo wa ujenzi ulioanzishwa na viongozi wa kabla yake. Amesisitiza kuwa hakuna nguvu yoyote ile inayoweza kusimamisha ujenzi wa bwawa hilo kwa kutumia nguvu. Ameongeza kuwa: "Kama baadhi ya nchi zitatumia makombora, wengine wanaweza kutumia mabomu lakini suala hilo halina maslahi kwetu."

Mwaka 2011 Ethiopia ilianza kujenga bwawa hilo juu ya maji ya Mto Nile na ujenzi huo unatambuliwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme katika maji ya Mto Nile barani Afrika.

Cairo inasema kuwa, ujenzi wa bwawa hilo juu ya Mto Nile ni hatari sana kwa usalama wa maji wa Misri na inatofautiana na Addis Ababa kuhusiana na kiwango cha maji yanayopaswa kuingia katika ardhi ya nchi hiyo kutokana na mto huo.

Serikali ya Misri inaitakidi kuwa asilimia 90 ya mahitaji ya maji ya nchi hiyo inadhaminiwa na maji ya Mto Nile na kwamba baada ya bwawa la An-Nahdha kujazwa maji kikamilifu nchi hiyo itakabiliwa na matatizo makubwa ya uhaba wa maji.  

Tags

Maoni