Oct 31, 2019 12:16 UTC
  • Ikhwani yaitaka UN kuokoa maisha ya kiongozi wake aliyoko katika jela ya Misri

Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri imeutaka Umoja wa Mataifa na taasisi zote za kisheria na za kutetea haki za binadamu za kikanda na kimataifa kuokoa maisha ya kiongozi wake, Dakta Mohammed Badie anayeshikiliwa katika jela ya Misri tangu mwaka 2013.

Taarifa ya harakati hiyo iliyotolewa leo Alkhamisi imeibebesha serikali ya Misri dhima ya uhai wa Dakta Mohammed Badie ambaye hali yake ya kiafya inadhoofika siku baada ya nyingine kutokana na manyanyaso na mateso makali.

Taarifa ya Ikhwanul Muslimin imesema kuwa, Badie anaendelea kushikiliwa katika seli ya mtu mmoja na amenyimwa nyenzo zote za maisha na wala haruhusiwi kukutana na jamaa zake kwa kipindi cha miaka mine sasa. Vilevile amezuiwa kukutana na wakili wake.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa jinai zinazofanywa na serikali ya Misri dhidi ya watu wasio na hatia yoyote, bila ya taasisi husika kuchukua hatua, hazitapita hivihivi bila ya hisabu na malipo dhidi ya wahalifu na watenda jinai hizo hapa duniani huko Akhera.

Awali binti wa kiongozi huyo wa Ikhwanul Muslimin alikuwa ametoa taarifa kuhusiana na hali mbaya ya baba yake katika seli ya jela ya Misri.

Dakta Mohammed Badie

Mohammed Badie ambaye alitiwa nguvuni baada ya kuondolewa madarakani serikali ya kwanza iliyochaguliwa kwa njia za kidemokrasia ya Muhammad Morsi nchini Misri hapo mwaka 2013, amehukumiwa kifo na vifungo mara kadhaa kwa tuhuma malimbali zinazohusiana na masuala ya kisiasa.  

Taasisi za kutetea haki za binadamu zinahofia kwamba, yumkini Dakta Mohammed Badie akakumbwa na hatima kama ile iliyomkuta rais wa zamani wa nchi hiyo Muhammad Morsi aliyeaga dunia katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa vyombo vya serikali ya Misri. 

Tags