Nov 10, 2019 07:23 UTC
  • Mfalme wa Morocco awaachia huru mamia ya wafungwa kwa mnasaba wa Maulidi

Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco ametangaza msahama kwa wafungwa 300 kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mazazi ya Mtume Muhammad (SAW).

Shirika rasmi la habari la Morocco MAP limeripoti kuwa, Mfalme wa Morocco amewaachia huru wafungwa hao, ambao baadhi yao walikuwa magerezani na wengine walikuwa wamechiwa huru kwa dhamana huku kesi zao zikiendelea, kwa mnasaba wa Maulidi ya Mtume Mtukufu (al-Mawlid al-Nabawi) (SAW).

Morocco kama aghalabu ya nchi nyingine za Kiislamu duniani, inatazamia kuadhimisha rasmi mazazi hayo ya Mtume SAW leo Jumapili, ingawaje shamrashamra hizo zilianza tokea jana katika mji wa Sale. Waislamu wa Palestina walifanya sherehe za Maulidi jana Jumamosi katika Ukanda wa Gaza.

Sherehe za Maulidi mjini Sale, Morocco

Maelfu ya Waislamu wa Yemen licha ya taharuki na ukosefu wa usalama walikusanyika katika Medani ya al-Sabeen mjini Sana'a jana Jumamosi katika maadhimisho hayo.

Waislamu wa Kisuni wanategemea baadhi ya riwaya katika kuamini kwamba Mtume Muhammad (SAW) alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal huku Waislamu wa madhehebu ya Shia wakiwa na riwaya nyingine nyingi zinazowafanya waamini kuwa Mtukufu huyo alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal.

Shamrashamra za kusherehekea Mazazi ya Mtume SAW Yemen

Kipindi cha kati ya tarehe hizo mbili kilitangazwa na Imam Khomeini (MA), Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ili kuleta umoja na mfungamano kati ya Waislamu bila kujali madhehebu zao. 

Tags

Maoni