Nov 11, 2019 11:35 UTC
  • Gambia yafungua faili la mauaji ya Warohingya katika mahakama ya ICJ

Gambia imewasilisha faili la kesi ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Warohingya katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).

Gambia imefungua faili hilo katika mahakama hiyo ya juu ya Umoja wa Mataifa iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi kwa niaba ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.

Mawakili wa Gambia wameiomba ICJ itoe agizo la kuchukuliwa hatua za dharura za kukomeshwa mauaji zaidi ya Waislamu wa Kirohingya.

Abubacarr Marie Tambadou, Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria wa Gambia amesema katika taarifa kuwa, "Gambia imechukua hatua hii ili kutafuta haki na kuhakikisha wahusika wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Myanmar dhidi ya Warohingya wanabebeshwa dhima."

Haya yanajiri siku chache baada ya maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kushughulikia jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini humo.

Askari wa Myanmar wanaowakandamiza Warohingya

Wito huo ulitolewa na ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, Yanghee Lee na Mwenyekiti wa Kamisheni Huru ya Kutafuta Ukweli kuhusu Myanmar, Marzuki Darusman ambao wanataka kuwekewa vikwazo makampuni yanayomilikiwa na jeshi la Myanmar na makamanda wa jeshi waliohusika na jinai kubwa dhidi ya binadamu na jinai za kivita dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuliwa, laki nane wamejeruhiwa na wengine wapatao milioni moja wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh ili kunusuru maisha yao, baada ya jeshi na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka kuanzisha mauaji ya kinyama Agosti 25 mwaka 2017.

Tags

Maoni