Nov 15, 2019 01:24 UTC
  • Nchi za Ulaya zaeleza wasiwasi wao kuhusu rekodi mbaya ya haki za binadamu ya Misri

Nchi kadhaa za Ulaya zimeishutumu serikali ya Misri kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, huku wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wakieleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza katika nchi hiyo inayoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Sisi.

Wawakilishi wa nchi mbalimbali zikiwemo wanachama wa Umoja wa Ulaya jana katika kikao cha msimu cha Umoja wa Mataifa cha kujadili hali ya haki za binadamu nchini Misri kilichofanyika mjini Geneva, Uswisi walikosoa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Misri chini ya utawala wa Rais Abdel Fattah al Sisi kwa kuwatesa watu, mauaji ya kiholela, kupotezwa kwa watu, mauaji ya umati, hali mbaya katika jela na seli za nchi hiyo na kuwakandamiza wanawake.

Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri  
 

Julien Braithwaite Balozi wa Uingereza amekiambia kikao hicho kuwa, wanasikitishwa na kutiwa wasiwasi na vizuizi vinavyowekwa na serikali ya Cairo dhidi ya watetezi wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuwatia mbaroni, kuwawekea marufuku ya kusafiri wanaharakati hao, kuzuia mali zao na vizuizi katika uga wa uhuru wa kujieleza, kufanya maandamano na mikutano ya amani.  

Kwa muda sasa Rais al Sisi wa Misri anakabiliwa na ukosoaji na lawama za jamii ya kimataifa kutokana na ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali yake dhidi ya makundi ya kiraia tangu aingine madarakani mwaka 2014. Abdel Fattah al Sisi alishika hatamu za uongozi wa Misri mwaka 2014 yaani mwaka mmoja baada ya kuongoza mapinduzi yaliyomng'oa madarakani Rais wa kwanza kuwahi kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini huko Mohamed Morsi. Morsi aliaga dunia mwezi Juni mwaka huu mjiniCairo akiwa mahakamani akisikiliza kesi iliyokuwa ikimkabili.  

Mwendazake, Mohamed Morsi, Rais halali wa Misri aliyepinduliwa na jeshi

 

Tags

Maoni