Nov 15, 2019 01:25 UTC
  • Congo yaanza kutoa chanjo mpya ya Ebola katika mji wa Goma

Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mpaka (MSF) imetangaza kuwa maafisa wa afya wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameanza kutoa chanjo mpya ya kudhibiti ugonjwa wa Ebola iliyotengenezwa na kampuni ya Johnson & Johnson.

Chanjo hiyo mpya ambayo imeidhinishwa katika majaribio ya kitaalamu itatolewa kwa watu elfu 50 katika mji wa Goma wenye jamii ya watu milioni mbili na uko katika mpaka wa Congo na Rwanda.

Chanjo hiyo inayotolewa kwa sindano mbili zinazopishana kwa wiki 8, inatolewa sambamba na ile iliyotongenezwa na kampuni ya Merck inayotolewa kupitia sindano moja. Chanjo hii ya Merck imekwishatolewa kwa watu laki mbili na nusu tangu ugonjwa wa Ebola uliporipuka mashariki mwa nchi hiyo mwezi Agosti mwaka jana.

Chanjo ya Ebola

Karibu watu 2,200 wamepoteza maisha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na mlipuko huo wa ugonjwa wa Ebola.

Maafisa wa sekta ya afya wa Congo DR wamekosoa chanjo mpya ya J&J wakisema haijafanyiwa majaribio ya kutosha licha ya kuidhinishwa na Shirika la Afya Dunia (WHO).  

Mbinu mpya zinazotumiwa na maafisa wa afya ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo vimesaidia kudhibiti mlipuko wa ugonwja wa Ebola huko mashariki mwa Congo ambao ndio mbaya zaidi duniani baada ya ule wa mwaka 2013 hadi 2016 ulioua watu zaidi ya 11,300 huko magharibi mwa Afrika.

 

Tags

Maoni