Nov 17, 2019 11:26 UTC
  • Watu kadhaa wauawa licha ya uchaguzi mdogo kufanyika chini ya ulinzi mkali nchini Nigeria

Watu kadhaa wameuawa licha ya uchaguzi wa magavana wa majimbo mawili ya Nigeria kufanyika chini ya ulinzi mkali.

Jana wananchi wa Nigeria walikwenda kwenye masanduku ya kupigia kura kuchagua magavana wa majimbo mawili ya Bayelsa na Kogi;  uchaguzi mdogo ambao umefanyika chini ya ulinzi mkali. Jimbo la Bayelsa liko kwenye eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la kusini mwa Nigeria huku lile la Kogi likiwa katikati ya nchi hiyo yenye watu wengi ya magharibi mwa Afrika.

Hata hivyo, licha ya kuwekwa ulinzi mkali, kumetokea machafuko kwenye uchaguzi huo na kupelekea watu kadhaa kuuawa kwenye vituo vya kupigia kura.

Safu ya wapiga kura Nigeria

 

Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, ofisi zinazoshughulikia upigaji kura zilichelewa kufunguliwa kwa nusu saa katika jimbo la Bayelsa.

Wakati zoezi la kupiga kura likiwa linaendelea, helikopta za polisi ziliruka kwenye vituo vya kupigia kura huku maafisa wa polisi na wanajeshi waliojizatiti kwa nguo za kupambana na fujo wakiwa wamemiminwa kwenye maeneo nyeti ya majimbo hayo.

Itakumbukwa kuwa jimbo la Bayelsa ni ngome ya wapinzani na hasa chama kikuu cha upinzani cha People's Democratic Party (PDP) kinachoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan.

Tags

Maoni