Nov 21, 2019 01:05 UTC
  • Tunisia yatahadharisha kuhusu taathira za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imetahadharisha kuhusu taathira hatari za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia jana ilitahadharisha kuhusu athari hatari za kuhalalisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria kwa visingizio na hali zozote zile. Aidha imesema kuwa ujenzi huo wa vitongoji unakiuka makubaliano na maazimio ya kimataifa.  

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imetoa taarifa na kusisitiza kuhusu msimamo wake wa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kurejeshwa haki zote halali za wananchi hao; kukiwemo kuasisiwa serikali huru ambayo mji wake mkuu ni Quds Tukufu. 

Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Jumatatu alidai kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan si ukiukaji wa sheria za kimataifa. 

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani

Hatua ya Marekani ya kuunga mkono ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina imelalamikiwa na kukosolewa  na wananchi wa Palstina, Umoja wa Ulaya, Bunge la Kiarabu na nchi mbalimbali duniani.  Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Disemba 23 mwaka 2016 lilipasisha azimio nambari 2334 na kuutaka utawala wa Kizayuni kusitisha kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji hivyo tajwa katika maeneo wanayoishi raia wa Palestina. 

 

Tags

Maoni