Nov 27, 2019 14:07 UTC
  • Misri yarusha satalaiti ya mawasiliano katika anga za mbali

Misri imezindua satalaiti yake ya kwanza ya mawasiliano kwa kuirusha katika anga za mbali.

Baraza la Mawaziri nchini Misri limesema leo katika taarifa kuwa, satalaiti hiyo ya 'Tiba-1' ilirushwa katika anga za mbali jana jioni, na kwamba hatua hiyo itapiga jeki sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Satalaiti hiyo inayomilikiwa na kuelekezwa (kudhibitiwa) na serikali ya Cairo itaimarisha mawasiliano na hudumaa za intaneti nchini Misri, hususan katika maeneo ya vijijini.

Satalaiti hiyo ya Tiba-1 yenye uzito wa tani 5.6 ilizinduliwa na kurushwa katika anga za mbali kwa kutumia roketi la shirika la Ulaya la Arianespace, kutoka eneo la Guiana linalodhibitiwa na Ufaransa, kaskazini mashariki mwa pwani ya Amerika Kusini.

Satalaiti na sayari ya dunia

Inaarifiwa kuwa, satalaiti hiyo itaanza kufanya kazi miezi mitatu baada ya kuzinduliwa kwake. Mohamed El-Qousy, Mkuu wa Idara ya Anga za Mbali ya Misri amesema "Kuimarika kwa uchumi kunategemea mtandao madhubuti wa mawasiliano na Misri ipo katika njia hiyo. Uzinduzi huo ulipaswa kufanyika Jumatatu iliyopita lakini ukaakhirishwa kutokana na hali mbaya ya hewa."

Mapema mwezi huu, Sudan pia ilizindua kwa kurusha angani satalaiti yake ya kwanza itakayoshughulika na utafiti wa kijeshi, kiuchumi na wa tekonolojia ya anga za mbali. 

Tags

Maoni