Dec 07, 2019 07:15 UTC
  • Shambulizi la al-Shabaab dhidi ya basi la abiria laua 10 Kenya

Watu 10 wamethibitishwa kuuawa katika shambulizi dhidi ya basi la abiria linaloaminika kufanywa na genge la kigaidi na kitakfiri al-Shabaab katika kaunti ya Wajir, kaskazini mashariki mwa Kenya mpakani na Somalia.

Kamanda Mkuu wa Polisi katika kaunti hiyo, Stephen Ngetich amesema genge hilo la kigaidi jana jioni lilivizia na kulishambulia basi la Medina lililokuwa likielekea katika kaunti jirani ya Mandera, kati ya maeneo ya Kutulo na Wargadud, ambapo watu 10 wameuawa.

Amesema watu wengine kadhaa wamejeruhiwa, huku abiria kadhaa wakifanikiwa kutoroka. Manusura wanasema, baada ya wapiganaji waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kulisimamisha basi hilo, waliwaagiza abiria ambao sio wakazi wa maeneo hayo kuteremka chini, ambapo walifyatuliwa risasi kwa karibu na kuwaua.

Shambulizi hilo limefanyika chini ya mwezi mmoja baada ya wanachama wa genge hilo la ukufurishaji, kushambulia kituo cha polisi cha Dadajabula katika kaunti hiyo ya Wajir, wakiwa na lengo la kuwatorosha wanachama wake wawili waliokuwa wakizuiliwa katika kituo hicho. Hata hivyo maafisa usalama walifanikiwa kutibua hujuma hiyo.

Magaidi wakufurishaji wa al-Shabaab

Miaka mitano iliyopita, kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab  lenye makao makuu yake nchini Somalia lilifanya hujuma nyingine dhidi ya basi la wasafiri, na kuua 28 miongoni mwao. 

Kama ilivyokuwa katika shambulizi la jana, waliouawa katika hujuma hiyo ya miaka mitano iliyopita katika kaunti ya Mandera walikuwa Wakristo ambao sio wakazi wa asili wa maeneo hayo.

Viongozi wa Kiislamu nchini humo wamekuwa wakilaani hujuma za namna hiyo za al-Shabaab, zenye shabaha ya kupanda mbegu za chuki na kuwagawa wananchi katika misingi ya dini. 

 

Tags

Maoni