Dec 08, 2019 07:13 UTC
  • Rais wa Gambia aapa kuwaadhibu wafanyamagendo ya binadamu baada ya ajali mbaya ya boti

Rais Adama Barrow wa Gambia ameahidi kuwaadhibu wafanyamagendo ya binadamu, kufuatia vifo vya makumi ya watu waliozama baharini baada ya boti waliyoabiri ndani yake kupinduka katika pwani ya Mauritania wakati ikijaribu kufika barani Ulaya.

Akizungumza na taifa kupitia televisheni hapo jana, Rais wa Gambia amesema: "Kupoteza maisha ya vijana 60 baharini ni janga la kitaifa na jambo la kutia wasiwasi mkubwa kwa serikali yangu."

Ameongeza kuwa, uchunguzi kamili wa polisi umeanza kufanywa ili kujua kiini na chanzo cha janga hilo kubwa la kitaifa na kwamba waliohusika watashtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Watu wasiopungua 62 walighariki na kupoteza maisha siku ya Jumatano iliyopita katika pwani ya Mauritania, wakati boti iliyowabeba, ambayo ilikuwa ikielekea Visiwa vya Canary nchini Uhispania, ilipogonga jabali. 

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa kwa ajili ya Uhajiri (IOM), ajali hiyo imesababisha maafa makubwa zaidi yaliyosajiliwa rasmi ya vifo vya watu katika mwaka huu, kupitia kile kinachoitwa 'uhajiri wa magharibi'.

Wahajiri haramu wakitumia usafiri usio salama kwa safari za kuelekea Ulaya

Watu zaidi ya 80 walinusurika katika ajali hiyo baada ya kuogelea kuelekea fukwe za pwani ya Mauritania.

Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa kwa ajili ya Uhajiri liliripoti hapo jana kuwa boti nyingine iliyobeba watu kadhaa ilikamatwa siku ya Ijumaa katika bahari kuu ya Mauritania na askari wa gadi ya pwani ya nchi hiyo.

Abiria waliokuwemo ndani ya boti hiyo inayokadiriwa kubeba watu 150 hadi 180 walirejeshwa hadi mji wa Nouamghar, yapata kilomita 150 kaskazini mwa mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott na kupatiwa chakula na mablangeti.

Kwa mujibu wa IOM, watu 158 wamethibitika kufariki dunia katika mwaka huu, kulinganisha na 43 waliopoteza maisha yao mwaka uliopita wakati wakijaribu kufika Visiwa vya Canary nchini Uhispania.../

Tags

Maoni