Dec 09, 2019 08:08 UTC
  • Wanyamapori waua watu 96 nchini Tanzania

Watu zaidi ya 96 wameuawa na wengine 90 wamejeruhiwa kutokana na wanyamapori waliovamia mashamba na maeneo ya makazi nchini Tanzania tangu Julai mwaka 2018 hadi Julai mwaka 2019.

Hayo yamedokezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania Profesa Adolf Mkenda ambaye ameongeza kuwa idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa na wanyamapori imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Amesema hayo katika mkutano uliofanyika Mwanza kujadili njia bora za kudhibiti migongano kati ya binadamu na wanyamapori, huku akisema wanyamapori waliwaua watu 39 na kuwajeruhi wengine 37 kutoka Julai mwaka 2017 hadi Julai mwaka 2018.

Ametaja ndovu au tembo, simba, faru na mamba kuwa wanyamapori ambao wamekuwa chanzo kikuu cha mauaji hayo, huku akiongeza kuwa kutoka mwaka 2018 hadi 2019, wanyama hao wameharibu hekta 13.644 za mazao mashambani ikilinganishwa na hekta 637 za mwaka 2017 hadi 2018.

Simba katika mbuga ya wanyama, Nairobi Kenya

Kwa upande wake, mkurugenzi wa wanyamapori nchini Tanzania Meurus Msuha amesema wamekutana na wadau mbalimbali wakiwemo wahifadhi ili kukabiliana na changamoto ya muingiliano wa wanyamapori kwenye makazi ya watu.

Pato la utalii huchangia takribani asilimia 17.6 ya pato la taifa Tanzania na watalii wengi hutembelea mbuga za wanyamapori.

Tags

Maoni