Dec 09, 2019 11:07 UTC
  • Saudi Arabia ilimrubuni kwa fedha nyingi Omar al Bashir akatuma wanajeshi wa Sudan kwenye lindi la mauti nchini Yemen
    Saudi Arabia ilimrubuni kwa fedha nyingi Omar al Bashir akatuma wanajeshi wa Sudan kwenye lindi la mauti nchini Yemen

Wanajeshi wa Sudan ni miongoni mwa askari vamizi wanaoendesha mauaji dhidii ya Waislamu wa Yemen tangu Saudi Arabia ilipoivamia nchi hiyo ya Kiarabu takriban miaka mitano iliyopita. Baada ya kupita miaka yote hiyo ya jinai dhidi ya wananchi maskini wa Yemen, wavamizi wa nchi hiyo sasa wanakiri kwamba njia pekee ya kumaliza vita hivyo ni mazungumzo.

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok, mbali na kusisitiza kuwa, mgogoro wa Yemen utatuzi wake ni mazungumzo na wala si mashambulizi ya kijeshi amesema pia kuwa, idadi ya wanajeshi wa Sudan walioko Yemen wamepunguzwa kutoka 15 elfu na hivi sasa wamebakia elfu tano tu. 

Sudan ilijiingiza kwenye vita vya Yemen kufuata mkumbo wa Saudi Arabia tangu mwezi Machi 2015 tena katika hali ambayo kimsingi jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen hazikuwa tishio lolote la kiusalama kwa Sudan na wala walikuwa hawahatarishi manufaa ya kitaifa ya Khartoum. Kabla ya hapo pia, hakuna kundi lolote nchini Yemen lililokuwa na chuki na Sudan au lililokuwa limefanya jambo lolote la kuichokoza nchi hiyo. Kusema kweli wanajeshi wa Sudan walitumwa kuivamia Yemen kwa amri tu ya Jenerali Omar al Bashir, rais wa zamani wa Sudan aliyeng'olewa madarakani kwa hasira za wananchi. 

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok

 

Kilichofanywa na Jenerali al Bashir, ni kutaka kujinufaisha binafsi tu na kulinda utawala wake kwa njia yoyote ile ikiwa ni pamoja na kujipendekeza kwa Saudi Arabia na Marekani. Saudia ilimrubuni kwa fedha nyingi al Bashir na kumfanya aamue kutuma wanajeshi kwenda kufanya jinai dhidi ya Waislamu wa Yemen. Hata hivyo kujipendekeza kote huko hakukumfalia kitu al Bashir ambaye hivi sasa yuko korokoroni akisubiri hukumu zake.

Matukio ya Sudan yaliyopelekea kuingia madarakani Baraza la Mpito la Kijeshi yalitoa fursa ya kutangazwa idadi hasa ya wanajeshi wa Sudan walioko Yemen. Generali Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hemetti, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu wa Mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan baada ya kupinduliwa Jenerali Omar al Bashir alifichua kuwa, kuna wanajeshi 30 elfu wa Sudan nchini Yemen, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya wanajeshi walioshiriki kwenye muungano vamizi huko Yemen. Idadi hiyo ilitangazwa wakati ambapo wanajeshi wengi vamizi wa Sudan walikuwa wameshauawa.

Wanajeshi wa Sudan wakiwa katika mazingira magumu mno Yemen

 

Yahya Sarii, Msemaji wa Majeshi ya Yemen alisema kuwa, watawala wa Sudan wanacheza na roho za wanajeshi wao, kwani idadi ya wanajeshi mamluki kutoka Sudan waliouliwa na kujeruhiwa nchini Yemen tangu vilipoanza vita hivyo vya kivamizi walikuwa wameshapindukia 8,000. Wanajeshi 4253 walikuwa wameshauawa hadi wakati huo na waliobakia kati ya hao 8,000 walikuwa wamejeruhiwa. 

Pamoja na hali kuwa hivyo, wakuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan waliingia madarakani huko Sudan kwa msaada wa wavamizi wenzao, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao waliona hawawezi kumsaidia tena al Bashir mbele ya hasira za wananchi. Hivyo majenerali hao wa kijeshi wa Sudan nao wameendelea kuunga mkono kuweko wanajeshi mamluki wa Sudan nchini Yemen. Pamoja na hayo, Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok amesema kuwa, idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo watapunguzwa huko Yemen. Ametoa matamshi hayo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya wananchi wa Sudan ambao hawakufurahishwa hata kidogo na kutumwa wanajeshi wa nchi yao kwenda kufanya jinai dhidi ya Waislamu wenzao nchini Yemen tena bila ya sababu yoyote. Hivi sasa wananchi wa Sudan wanataka kurekebishwa makosa yaliyofanywa huko nyuma na njia bora kabisa kwa mtazamo wao ni kurudishwa nyumbani haraka wanajeshi wao wote waliotumwa Yemen. Wananchi wa Sudan wanaamini kuwa nchi yao imeingia katika ukurasa mpya wa kisiasa hivyo ni wajibu wake kuwa huru na kutoruhusu madola ajinabi kuathiri misimamo ya nchi yao.

Baadhi ya wanajeshi wa Sudan waliouawa nchini Yemen walikokwenda kuvamia bila ya sababu yoyote

 

Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa wa Sudan amesema: Hasira zimeenea katika kada zote za jamii ya Sudan kutokana na vitendo vya serikali ya mpito, na kwamba wananchi wa Sudan wanataka kurekebishwa makosa yote ya huko nyuma na muhimu kuliko yote ni makosa yaliyofanyika kuhusu vita vya Yemen, hivyo cha kufanya ni kukomeshwa mara moja vita hivyo. 

Katika upande mwingine, hivi sasa umuhimu wa kufanyika mazungumzo ya kutatua mgogoro wa Yemen unahisika zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Suala hilo limetiliwa mkazo pia na Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok. Hasa kwa kutilia maana kwamba sasa hivi wavamizi wa Yemen wakiongozwa na Saudi Arabia wanazidi kutengwa siku baada ya siku. Hivi sasa wavamizi hao wamekwama kwenye kinamasi nchini Yemen, na hawana njia nyingine isipokuwa kumaliza vita hivyo. Inaonekana wazi kuwa, kupunguzwa idadi ya wanajeshi wa Sudan ndani ya muungano vamizi wa Saudi Arabia ni sehemu ya hatua za wavamizi hao za kumaliza kimya kimya vita vya Yemen bila ya kukiri hadharani kwamba wameshindwa.

Tags

Maoni