Dec 09, 2019 12:24 UTC
  • Gavana wa Nairobi apandishwa kizimbani, akana mashtaka yanayomkabili

Gavana wa jiji la Nairobi nchini Kenya Mike Mbuvi Sonko, amekana mashtaka yanayomkabili, ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi unaohusisha mamilioni ya dola, wakati alipofikishwa mahakamani mapema leo.

Sonko alitiwa nguvuyni siku ya Ijumaa akituhumiwa pamoja na mambo mengine, kula njama ya kufanya ufisadi, kushindwa kufuata sheria zinazohusu taratibu za manunuzi na kumiliki mali ya umma kinyume cha sheria.

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka wa Kenya, DPP Noordin Haji amemtuhumu Mike Sonko na wasaidizi wake kuwa wamehusika na matumizi mabaya ya shilingi milioni 357 za Kenya, ambazo ni sawa na dola milioni 3.52 za Marekani.

DPP, Noordin Haji

Meya huyo wa jiji la Nairobi ambaye ni mwanachama wa chama tawala cha Jubilee, alisema katika taarifa aliyotoa hapo jana kuwa, kukamatwa kwake kumetokana na sababu za kisiasa na kwamba yeye ni raia anayetii sheria.

Kupitia taarifa yake hiyo iliyoandikwa kwa lugha mbili za Kiingereza na Kiswahili, Sonko amewahimiza wafuasi wake wajiepushe na vitendo ambavyo amesema "vinaweza kuhatarisha amani".

Aidha amesema, anawaomba wafuasi wake na hata maadui zake pia wamuombee dua.

Katika kesi hiyo iliyosikilizwa na hakimu mkazi mkuu Douglas Ogoti, gavana huyo wa jiji la Nairobi amewakilisha na jopo zito la mawakili wa Kenya, akiwemo kiongozi wa waliowengi katika Baraza la Seneti, Kipchumba Murkomen.

Sonko ni maarufu kwa mitindo yake maalumu ya mavazi, aina kwa aina za vito vya dhahabu anavyovaa na mikato yake maalumu ya nywele.

Polisi waliweka vizuizi na ulinzi mkali katika eneo linalozunguka mahakama ili kuzuia kutokea fujo baada ya wafuasi wa gavana huyo kutoa mwito wa kufanya maandamano.../

Tags

Maoni