Dec 10, 2019 12:01 UTC
  • Tahadhari kuhusu ongezeko la mahitaji ya misaada ya chakula eneo la Sahel Afrika

Taasisi ya Kuzuia Migogoro ya Njaa imetangaza kwamba, idadi ya watu wanaohitajia misaada ya chakula imeongezeka maradufu katika eneo la Sahel Afrika kutokana na kuongezeka hali ya ukosefu wa amani na mapigano katika nchi za eneo hilo.

Mtandao wa Kuzuia Migogoro ya Chakula unaofanya kazi chini ya Shirika la Ushirikiano na Ustawi wa Kiuchumi (OECD) lenye makao yake Paris nchini Ufaransa umetangaza kuwa, idadi ya watu wanaohitajia misaada ya chakula katika nchi 16 za eneo la Sahel barani Afrika imeongezeka mara mbili mwaka huu wa 2019 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake na sasa imefikia watu milioni 9 na laki 4. 

Mtandao huo unakadiria kwamba, hadi mwezi Juni mwaka ujao wa 2020 idadi ya watu wanaohitajia misaada ya chakula katika eneo hilo itaongezeka zaidi na kufikia milioni 14 na laki 4. 

Njaa inasumbua nchi nyingi za Sahel Afrika

Taarifa ya Mtandao wa Kuzuia Migogoro ya Chakula imetolewa katika mkutano uliohudhuriwa na wataalamu wa taasisi hiyo wakishirikiana na wawakilishi wa nchi za Kiafrika zinazosumbuliwa na uhaba wa chakula, mashirika ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za wahisani.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa machafuko na ukosefu wa amani ndiyo sababu kuu ya ongezeko la wakimbizi, upungufu wa chakula na kadhalika. Imesisitiza kuwa nchi za Nigeria, Niger na Burkina Faso ndizo zinazosumbuliwa zaidi na njaa na uhaba wa chakula.   

Maoni