Dec 11, 2019 01:15 UTC
  • Qatar Airways kuchukua asilimia 60 ya hisa za uwanja wa ndege wa Rwanda

Shirika la Ndege la Qatar Airways limeafiki kuchukua asilimia 60 ya hisa katika uwanja mpya wa kimataifa wa ndege nchini Rwanda ambao unatazamiwa kugharimu dola bilioni 1.3.

Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baina ya pande mbili, sehemu ya kwanza ya uwanja huo wa ndege itakuwa na jengo lenye uwezo wa kuhudumia wasafiri milioni saba kwa mwaka. Uwanja huo wa ndege utajengwa katika wilaya ya Bugesera, yapata kilimota 25 kusini magharibi mwa mji mkuu, Kigali.  Sehemu ya pili ya uwanja huo inatazamiwa kumalizika mwaka 2032 ambapo uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumua wasafiri milioni 14 kwa mwaka.

Serikali ya Rwanda imesema mapatano hayo yataliwezesha shirika la ndege la Qatar Airways kujenga, kumiliki na kusimamia uwanja huo wa ndege wa kisasa.

Picha ya kompyuta ya uwanja wa ndege unaopangwa kujengwa na Qatar Airways nchini Rwanda

Waziri wa Miundo Msingi wa Rwanda Claver Gatete amewaambia waandishi habari kuwa bado wanatafuta shirika ambalo litajenga uwanja huo.

Jumatatu Mfalme wa Qatar Sheikh Sheikh Tamim Bin Hamad Al Thani alitembelea Rwanda kushiriki katika kikao cha kimatiafa cha kupambana na ufisadi ACE. Hii ni safari ya pili ya mfalme wa Qatar nchini Rwanda baada ya safari yake ya siku tatu nchini humo mwezi Aprili.

 

Maoni