Dec 13, 2019 00:43 UTC
  • Watu milioni 5.5 katika hatari ya kufa njaa Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu milioni tano na laki tano wanakabiliwa na baa la njaa nchini Sudan Kusini, kutokana na ukame na mafuriko ya hivi karibuni yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limesema linahitaji dola milioni 270 za dharura ili kuyanusuru maisha ya mamilioni ya Wasudan Kusini wanaokodolewa macho na njaa.

Matthew Hollingworth, Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Iwapo hatua za dharura na za makududi hazichukuliwa, basi taifa hilo changa zaidi barani Afrika litakabiliwa na janga kubwa la njaa mwaka ujao 2020. Lazima tufikishe misaada ya kibinadamu kwa wanaohitaji katika maeneo kame na maeneo ambayo yameathiriwa na mafuriko."

Afisa huyo wa WFP nchini Sudan Kusini ambaye alizungumza na Reuters kupitia njia simu akiwa Juba jana Alkhamisi ameeleza bayana kuwa, watu milioni moja wameathiriwa moja kwa moja na mafuriko nchini humo.

Amesema utapiamlo wa kiwango cha juu miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano umeongezeka kutoka asilimia 13 mwaka jana, hadi asilimia 16 mwaka huu.

Watoto ndio wahanga wakuu wa baa la njaa Sudan Kusini

WFP inasisitiza kuwa, machafuko yanayoendelea nchini Sudan Kusini yanazuia shughuli za kugawa misaada ya chakula kwa watu wanaosumbuliwa na njaa kali katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya milioni 821 katika pembe mbalimbali za dunia wanakabiliwa na baa la njaa na kwamba ni muhali kufikia dira ya Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ya kutokomeza baa la njaa duniani kikamilifu kufikia mwaka 2030.

 

Tags

Maoni