Dec 13, 2019 03:58 UTC
  • Haftar atangaza 'mapigano ya kuamua mshindi na mshinde' ya kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli

Kamanda wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA), Khalifa Haftar ametangaza kuanza kile alichokiita 'mapigano ya kuamua mshindi na mshinde' ya kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Haftar ametoa tangazo hilo baada ya kupita miezi minane tangu alipoanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya mji huo kwa lengo la kunyakua udhibiti wake kutoka mikononi mwa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa (GNA) inayotambuliwa rasmi kimataifa.

"Muda umewadia wa shambulio kubwa na la kila upande linalotarajiwa na kila Mlibya huru na mkweli" amesisitiza jenerali huyo mwasi katika tangazo alilotoa hapo jana kwa njia ya televisheni na kuongezea kwa kusema: "Leo, tunatangaza mapigano ya kuamua mshindi na mshinde na kusonga mbele kuelekea kitovu cha mji mkuu ili kuukomboa... songeni mbele sasa hivi mashujaa wetu."

Khalifa Haftar ametoa tangazo hilo huku Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ikisisitiza jana hiyo hiyo kwamba hali ya mambo "iko chini ya udhibiti" na kwamba vikosi vya serikali hiyo vimejizatiti katika ngome zao kusini mwa mji mkuu huo wa Libya.

Wapiganaji wanaoiunga mkono GNA

Waziri wa Mambo ya Ndani wa GNA, Fathi Bashagha ametangaza kupitia kanali ya televisheni ya al-Ahrar kwamba, wako tayari kuzima jaribio lolote jengine la kiwendawazimu litakalofanywa na Haftar ili kuiangusha serikali hiyo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, raia wasiopungua 200 na wapiganaji zaidi ya 2,000 wameuawa tangu wapiganaji watiifu wa Haftar wa LNA walipoanzisha hujuma na uvamizi dhidi ya Tripoli. Hujuma hiyo ya kijeshi imesababisha pia watu wapatao 146,000 wabaki bila makazi.

Kundi la LNA linaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya madola ya Magharibi.../

 

 

Maoni