Dec 13, 2019 13:36 UTC
  • Mapigano makali yashuhudiwa karibu na uwanja wa ndege wa Tripoli, Libya

Askari wa serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya wameshambuliana vikali na wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar katika viunga vya uwanja wa ndege wa Tripoli.

Mapigano hayo kati ya askari wa serikali ya umoja wa kitaifa na wale wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar kusini mwa mji wa Tripoli, yamejiri katika hali ambayo kwa mujibu wa duru za habari, pande hizo zimeshadidisha vita kati yao. Wakati huo huo askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya wamefanikiwa kudhibiti eneo la Al Toggar sambamba na kuangamiza magari manne ya deraya mali ya Imarati katika eneo hilo.

Wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar, wanaosaidiwa na Saudia, Misri, Marekani na Imarati  katika kumwaga damu za Walibya

Kundi la wapiganaji linalojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' linaloongozwa na Khalifa Haftar na ambalo kwa miaka kadhaa limekuwa likidhibiti eneo la mashariki mwa Libya, miezi ya hivi karibuni limesonga mbele kuelekea kaskazini mwa nchi hiyo. Kundi hilo linaungwa mkono na Saudia, Misri, Imarati, Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi. Aidha tarehe nne Aprili mwaka huu, Haftar akiongoza askari wake alishambulia mji wa Tripoli, ambao ndio makao makuu ya serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj, kitendo ambacho kilikabiliwa na radiamali kali kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Tags

Maoni