Dec 14, 2019 03:39 UTC
  • Ndege za jenerali muasi zafanya mashambulizi makali Misrata Libya

Ndege za kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na jenerali muasi, Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudia, Imarati, Misri na baadhi ya nchi za Magharibi, zimefanya mashambulizi makali katika mji wa Misrata wa kaskazini mwa Libya.

Vyombo vya habari vimetangaza habari hiyo usiku wa kuamkia leo ingawa havikusema mashambulizi hayo yamesababisha hasara kiasi gani.

Jenerali Khalifa Haftar na jeshi lake wanadhibiti eneo la mashariki mwa Libya na tangu mwezi Aprili mwaka huu alianzisha mashambulizi makubwa ya pande zote dhidi ya mji mkuu Tripoli kwa tamaa ya kuuteka mji huo na kujitangaza kiongozi mkuu wa Libya. Hata hivyo ndoto hiyo hadi hivi sasa imeshindwa kuaguliwa. Haftar alianzisha mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli mara baada ya kutembelea Saudi Arabia na kuonana na viongozi wa ngazi za juu wa ukoo wa Aal Saud.

Jenerali muasi Khalifa Haftar wa Libya alipoonana na viongozi wa ngazi za juu ya Saudi Arabia kabla ya kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya mji wa Tripoli ambayo hadi sasa yameshapelekea zaidi ya watu 1090 kuuawa

 

Hata hivyo mashambulizi hayo ya Jenerali Khalifa Haftar hadi hivi sasa yanalaaniwa na jamii ya kimataifa ambayo inaitambua serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj kuwa ndiyo serikali halali nchini Libya. 

Tangu jenerali huyo muasi aanzishe mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli kwa msaada wa kila upande wa Saudia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na baadhi ya nchi za Magharibi hadi hivi sasa amesababisha zaidi ya watu 1090 kuuawa na wengine wasiopungua 5700 kujeruhiwa. 

Libya haijawahi kushuhudia utulivu wa angalau siku moja tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kumpindua kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi. Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani ziliingilia kampeni hiyo, na kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu nchini Libya na baadaye kuitelekeza nchi hiyo huku silaha zikiwa zimeenea mikononi mwa makundi hasimu.

Maoni