Dec 14, 2019 11:07 UTC
  • Kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais Algeria katika kivuli cha maandamano ya upinzani

Uchaguzi wa Rais Algeria umefanyika katika anga iliyogubikwa na ukosefu wa amani na usalama. Ripoti zinasema nusu ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura ndio walioshiriki kwenye zoezi hilo.

Tume Huru ya Uchaguzi ya Algeria imetangaza kuwa katika uchaguzi huo Abdelmajid Tebboune mmoja wa mawaziri wakuu wa utawala wa Bouteflika amechaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo baada ya kupata asilimia 58.15 ya kura. 

Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Algeria ametangaza kuwa asilimia 41.13 ya wananchi wameshiriki  katika uchaguzi huo wa rais na kueleza kuwa, Abdelmajid Tebboune ameshinda kiti cha rais kwa kuibuka na ushindi wa kura milioni nne laki tisa na elfu 45 na 116. Abdulqadir Bengrina Mkuu wa Harakati ya El Binaa ameshika nafasi ya pili baada ya Tebboune na Waziri Mkuu wa zamani wa Algeria Ali Benflis ameshika nafasi ya tatu. Wagombea wengine Izzudin Mihoubi ambaye ni Katibu Mkuu wa chama cha Democratic National Rally ameshika nafasi ya nne na Abdulaziz Belaid, Mwenyekitii wa chama cha al Mustaqbal ameambulia nafasi ya tano katika uchaguzi huo. Uchaguzi huo ni wa kwanza wa rais kufanyika Algeria baada ya kuondoka madarakani aliyekuwa rais wa wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika Aprili Pili mwaka huu. 

Wagombea watano wa uchaguzi wa rais Algeria

Katika miezi kumi iliyopita Algeria imekuwa katika ghasia na maandamano ya mara kwa mara ya wananchi waliokuwa wakipinga zoezi hilo la uchaguzi wa rais. Waandamanaj hao wanasema hakukuwepo mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki. Wananchi wengi wa Algeria wanataka kuuzuliwa maafisa wote wa serikali wenye mfungamano ya serikali iliyondoka madarakani ya Abdelaziz Bouteflika ambayo wanasema ilitawaliwa na ufisadi. Wapinzani hao wanataka kufanyike mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa siasa wa Algeria. Wanasema kufanyika uchaguzi wa rais katika mazingira ya sasa na ukishirikisha maafisa wa serikali iliyoondolewa madarakani kwa mashinikizo ya wananchi ni kudumisha utawala fasidi na mbovu. Kwa msingi huo vyama vingi vya siasa vya Algeria vimesusia uchaguzi huo. 

Katika mkondo huo zaidi ya vyama 30 vya siasa, jumuiya na mashirika ya wafanyakazi na masuala ya kijamii na shakhsia 120 huru na mashuhuri wakiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu kabla ya uchaguzi wa sasa walitoa taarifa ya pamoja wakiwataka wananchi wasusie uchaguzi huo. Taarifa hiyo ilisema kuwa, kufanyika uchaguzi wa rais katika mazingira ya sasa ni sawa na mchezo wa kuigiza, na lengo la wagombea 5 wanaochuana ni kulinda utawala fasidi na kidikteta wa Algeria. 

Waalgeria wanapinga matokeo ya uchaguzi wa rais

Pamoja na hayo uchaguzi wa rais wa Algeria umefanyika katika katika anga ya mzozo na mvutano mkubwa na Abdelmajid Tebboune amechaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo. Katika hotuba yake ya kwanza baada ya uchaguzi huo, Tebboune ameahidi kufanya marekebisho yanayosisitizwa na wananchi na kwamba anao uwezo wa kufanya mabadiliko hayo. Hata hivyo maandamano dhidi ya uchaguzi huo yangali yanaendelea. Baada tu ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Algeria wapiznani walifanya maandamano wakipiga nara zinazosema: "Hatutaki uchaguzi wa magenge", na wamemtaja mshindi wa uchaguzi huo kuwa ni rais aliyesimikwa na wanajeshi. Waandamanaji hao wametoa wito wa kufutwa matokeo ya uchaguzi huo. 

Kwa hali hii inaonekana kuwa, Abdelmajid Tebboune atalazimika kusalimu amri mbele ya baadhi ya matakwa ya wananchi na kufanya mabadiliko katika mfumo wa kisiasa wa Algeria. Vilevile inatazamiwa kuwa atawaachia huru wafungwa wa kisiasa kama njia ya kutulia hasira na maandamano ya wapinzani na kulazimika kufanya mazungumzo na kambi ya upinzani.

Kwa kutilia maanani haya yote inaonekana kuwa, Rais mteule wa Algeria anasubiriwa na kibarua kigumu na misukosuko mingi.    

Tags

Maoni