Dec 14, 2019 13:00 UTC
  • Al Bashir wa Sudan ahukumiwa kifungo cha miaka miwili katika kituo cha marekebisho

Rais wa zamani wa Sudan Omar al Bashir amehukumiwa kifungo cha miaka miwili katika kituo cha marekebisho ya kitabia baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu wa fedha na ufisadi.

Hii ni kesi ya kwanza kati ya kesi zingine kadhaa ambazo dikteta huyo wa zamani anakabiliwa nazo tokea apinduliwe baada ya kuitawala Sudan kwa karibu miaka 30.

Katika hukumu ambayo imetolewa Jumamosi na mahakama mjini Khartoum, al Bashir amepatikana na hatia ya kumiliki kinyume cha sheria fedha za kigeni, kupata fedha kinyume cha sheria na ufisadi.

Jaji al Sadiq Abdelrahman amesema: "Mahakama imempata Ombar Hassan al Bashir na hatia na imeamua kumpeleka katika kituo cha kijamii cha urekebishaji tabia kwa muda wa miaka miwili." Jaji huyo ameongeza kuwa: "Kwa mujibu wa sheria, wale ambao wamepindukia umri wa miaka 70 hawawezi kuhukumiwa kifungo jela."

Aidha jaji huyo amesema Bashir, 75, ataanza kuhudumu kifungo hicho baada ya kutolewa hukumu ya kesi nyingine kuhusu kuamuru mauaji ya waandamanaji katika maandamano yaliyopelekea atimuliwe madarakani.

Fedha taslimu ambazo zilipatikana ndani ya nyumba ya al Bashir baada ya kupinduliwa

Bashir alikuwa anakabiliwa na shtaka la kumiliki fedha taslimu zaidi ya dola milioni 130 zilizopatikana ndani ya nyumba yake. Hali kadhalika rais huyo wa zamani alikuwa anakabiliwa na shtaka la kupokea fedha taslimu dola milioni 25 kutoka kwa Mrithi wa Ufalme wa Saudia Mohammad bin Salman.

Omar Hassan al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo tarehe 11 Aprili mwaka huu kufuatia maandamano na malalamiko ya miezi kadhaa ya wananchi. Maandamano hayo yalichochewa na hali mbaya ya uchumi, ufisadi mkubwa na utumiaji mbaya wa madaraka wa al Bashir.

 

Tags

Maoni