Dec 14, 2019 16:06 UTC
  • Kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba: Sikumkamata Maalim Seif kwa kuwa hakufanya kosa lolote kwenye mikutano yake

Kamanda Polisi wa Mkoa wa Kaskazini kisiwani Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan amesema mahojiano yaliyofanywa na jeshi hilo kuwahusu viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, yanaonyesha kuwa walifanya mikutano yao bila ya kuvunja sheria.

Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi wa eneo hilo, uchunguzi unaonyesha kuwa hakuna kosa lililofanyika katika mikutano ya chama hicho. Amezidi kwenda mbali na kubainisha kwamba jeshi hilo halikuchukua hatua zozote dhidi ya Maalim Seif wakati wa ziara zake kwa sababu hakukuwepo na uvunjifu wa sheria wala hakukuwa na mikutano ya hadhara. Kwa mujibu wa kamanda huyo, polisi walifika katika maeneo ambayo Maalim Seif alifanya mikutano yake na hakuna sehemu ambayo kulibainika kufanyika mikutano ya hadhara zaidi ya ile ya ndani.

Maalim Seif

Alisema wanachama wa ACT-Wazalendo walikuwa wameketi kwenye viwanja vya ofisi zao vilivyozungushiwa uzio maalumu kuonyesha ni mikutano ya ndani. Wakati huo huo Maalim Seif Sharif Hamad amehoji sababu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kushangaa polisi kutozuia mikutano yake anayoifanya kisiwani Pemba, kama ambavyo pia amehoji sababu ya waziri huyo kutohoji mikutano ya Katibu Mkuu wa Chama Tawala CCM, Dk Bashiru Ally huko kisiwani Pemba, na kuongeza kuwa, "Kwanini Dk Bashiru alipotembelea Pemba na wafuasi wa CCM na kufanya maandamano na mikutano ya hadhara hakuchukua hatua.?" Amesema. Aidha kiongozi huyo wa kisiasa wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo amekosoa vikali amri ya Masauni kuwahusu makamanda wa jeshi la polisi aliotaka kufutwa kazi. Maali Seif amedai kuwa kile kinachoendelea hivi sasa ni wasiwasi uliopo ndani ya CCM na SMZ kuhusu nguvu ya ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni 

Awali Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kumuondoa na kumshusha cheo Sheikhan na kamanda wa Mkoa wa Kusini  kisiwani Pemba, Hassan Nassir Ally kutoka na kushindwa kwao kumchukulia hatua Maalim Seif. Naibu waziri huyo alitaka wachukuliwe hatua kwa sababu walishindwa kuzuia mikutano ya Maalim Seif pamoja na kutojengwa nyumba za polisi kisiwani Pemba licha ya Serikali kutoa maagizo.

 

 

 

 

Tags

Maoni