Dec 31, 2019 07:38 UTC
  • Al-Qaeda yakiri kuhusika na shambulizi la bomu lililoua 90 Somalia

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lililojitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaida limekiri kuhusika na shambulizi la bomu lililotokea mwishoni mwa wiki katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Ali Mohamud Rage, msemaji wa al-Shabaab amesema katika ujumbe wa sauti kuwa, "Mlipuko huo ulilenga vikosi vya Uturuki na Somalia na vilipata pigo kubwa." Raia wawili wa Uturuki ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo linalotajwa kuwa baya zaidi nchini Somalia ndani ya miaka miwili iliyopita.

Msemaji huyo wa al-Shabaab ameituhumu Uturuki kuwa inafyonza rasilimali za nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kwamba genge hilo la kigaidi litaendelea kulenga askari na raia wa Uturuki. Wahandisi kadhaa wa Kituruki wanaohusika na ujenzi wa barabara jijini Mogadishu walikuwapo katika eneo la tukio siku ya Jumamosi wakati wa mripuko huo.

Wakati huohuo, Idara ya Kiintelijensia ya Somalia (NISA) bila kutaja taifa lolote imesema nchi ajinabi ilipanga mauaji hayo ya umati jijini Mogadishu Disemba 28. Katika miaka ya hivi karibuni, Somalia imekuwa medani ya makabiliano ya kidiplomasia baina ya Uturuki na Qatar kwa upande mmoja, na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa upande mwingine.

Hujuma za al-Shabaab zimekuwa zikijiri kila uchao mjini Mogadishu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na nchi nyingi duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimelaani mripuko huo wa gari lililokuwa limeshehenezwa mabomu na kuua kigaidi zaidi ya watu 90 na kujeruhi wengine wengi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Genge la ukufurushaji la al-Shabaab limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara kama hayo ndani na nje ya Somalia.

Tags