Jan 16, 2020 02:32 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia amjibu Trump anayelilia Tuzo ya Nobel

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amejibu matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani aliyedai hivi karibuni kuwa yeye ndiye aliyepaswa kupewa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka jana 2019 na kusisitiza kuwa, Trump anapaswa kuwasilisha malalamiko yake kwa Kamati Andalizi ya Tuzo ya Nobel na sio kwa taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Akijibu bwabwaja hizo za Trump akiwa ziarani nchini Afrika Kusini, Abey Ahmed ameeleza bayana kuwa, “Rais Trump alipaswa kuwalalamikia waandaaji wa Tuzo ya Nobel,  na sio kuelekeza malalamiko yake kwa Ethiopia.

Waziri Mkuu wa Ethiopia amebainisha kuwa, "Binafsi sifahamu ni vigezo gani vinatumika kumchagua mshindi wa tuzo ya Nobel, kwa hivyo simuelewi anapoilalamikia Ethiopia."

Trump katika mkutano wa kisiasa huko Ohio hivi karibuni alidai kuwa, "Nilifanya makubaliano fulani, nikaiokoa nchi moja, lakini nikasikia kwamba kiongozi wa nchi hiyo amepewa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kuiokoa nchi hiyo.”

Licha ya kuwa Rais wa Marekani hakutaja wazi wazi jina la Ethiopia wala la Ahmed Abiy katika matamshi hayo, lakini kauli yake hiyo imepingwa vikali nchini Ethiopia.

Rais Donald Trump

Waziri Mkuu wa Ethiopia mwezi Oktoba mwaka uliopita alishinda Tuzo hiyo ya Amani ya Nobel kwa mwaka huo wa 2019 kutokana na juhudi zake za kuleta amani zilizopelekea kuhitimishwa mzozo na uhasama wa miongo miwili kati ya nchi mbili za Ethiopia na Eritrea.

Septemba mwaka jana pia, Trump alidai kuwa, "Ningepaswa kupewa Tuzo ya Nobel kutokana na mambo mengi sana niliyoyafanya iwapo wangeitoa tuzo hiyo kwa uadilifu, lakini hawafanyi hivyo." Trump amekuwa akidai mara kwa mara kuwa anapaswa kutunukiwa tuzo hiyo ya kifahari, licha ya kuandamwa na wimbi la ukosoaji nje na ndani ya nchi, kutokana na uongozi na sera zake mbovu.

Tags

Maoni