Jan 17, 2020 12:20 UTC
  • Kenya yatakiwa itangeze uvamizi wa nzige wa jangwani kuwa maafa ya kitaifa

Serikali ya Kenya imetakiwa kutangaza uvamizi mkubwa wa nzige wa jangwnai nchini humo kuwa ni maafa ya kitaifa kutokana na uharibifu mkubwa unaosababishwa na wadudu hao.

Wito huo umetolewa na  Mkuu wa Kilimo katika Kaunti ya Wajir Ahmed Sharrif ambaye amesema kufuatia uharibifu uliosababishwa na nzige wa jangwani, serikali inapaswa kutangaza uvamizi wa nzige hao kuwa janga la kitaifa ili fedha zaidi zitengwe kwa ajili ya kukabiliana nao.

Nzige wa jangwani wamevamia baadhi ya maeneo nchini Kenya tangu mwezi Disemba. Kati ya maeneo ya kwanza kuvamiwa ni kaunti ya Wajir inayopakana na Somalia. Nzige hao wamesababisha uharibifu mkubwa kwa mimea na miti. Miongoni mwa maeneo mengine yaliyoathiriwa ni Mandera, Marsabit na Isiolo, Meru, Samburu na Laikipia. Wataalamu wa Mazingira wanasema mabadiliko ya tabianchi ndiyo sababu kuu ya uvamizi wa nzige hao ambao waliingia Kenya wakitokea Somalia na Ethiopia.

Ndege ikitumika kusambaza kemikali ya kukabiliana na nzige nchini Kenya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limeonya kuwa nzige hao wa jangwani wanatazamiwa kuhujumu kaunti za Baringo na Turkana.

Serikali ya Kenya imewahakikishia wananchi kuwa imeweka mikakati ya kutosha kukabiliana na nzige wa jangwani.

Tayari ekari 175,000 za mashamba katika mataifa ya Somalia na Ethiopia, zimeharibiwa na nzige hao katika uvamizi mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya miaka 70, kwa mujibu wa FAO. Serikali ya Kenya imeagiza maelfu ya lita za kemikali za kukabiliana na wadudu hao pamoja na ndege za kunyunyizia dawa. 

 

Tags

Maoni