Jan 17, 2020 12:44 UTC
  • Mkuu wa Shirika la Usalama wa Taifa la Sudan afutwa kazi baada ya uasi

Mkuu wa Shirika la Usalama wa Taifa la Sudan amefutwa kazi baada ya jaribio lililofeli la mapinduzi ambalo lilitekelezwa na maafisa kadhaa wa usalama

Kwa mujibu wa taarifa, Abdel Fattah al Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan ametangaza kuwa, amemfuta kazi mkuu wa Shirika la Usalama wa Taifa Mustafa Dumblab na mahala pake pamechukuliwa na Jamal Abdul Majeed.

Aidha Baraza la Utawala la Sudan limetaka kufanyike mabadiliko ya kimsingi katika Shirika la Usalama wa Taifa.

Mapema Jumanne, Jeshi la Sudan lilitangaza kuwa, kufuatia uasi wa maafisa kadhaa wa Shirika la Usalama wa Taifa katika mji mkuu Khartoum, kulisikika milio ya risasi katika kituo kimoja cha shirika hilo kilicho karibu na Uwanja wa Ndege wa Khartoum jambo ambalo lilipelekea kufutwa safari za ndege na barabara za kuelekea katika uwanja huo.

Abdel Fattah al Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan

Msemaji wa Vikosi vya Kijeshi vya Sudan Jenerali Amer Mohamed Al-Hassan ametangaza kupinga uasi wa maafisa hao wa Shirika la Usalama wa Taifa na kusema walikuwa wanalalamikia mishahara na marupurupu yao.

Imearifiwa kuwa maafisa wa usalama waliokuwa wameanzisha uasi huo wanafungamana na rais aliyetimuliwa madarakani Omar al Bashir. Wanajeshi wawili waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa wakati walipokuwa wanazima uasi wa maafisa hao wa usalama.

Tags

Maoni