Jan 21, 2020 07:41 UTC
  • Serikali: Tutamkamata na kumshtaki Yahya Jammeh akirejea Gambia

Serikali ya Gambia imetishia kumkamata na kumfungulia mashitaka rais wa zamani wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani Yahya Jammeh iwapo atatia mguu nchini humo kutoka uhamishoni Equatorial Guinea.

Waziri wa Sheria, Abubacarr Tambadou amempa onyo kali rais huyo wa zamani wa Gambia, akisisitiza kuwa atakamatwa mara moja na kushitakiwa kwa jinai dhidi ya binadamu alizozitenda katika utawala wake wa zaidi ya miongo miwili.

Wiki iliyopita, wafuasi wa chama cha APRC cha Jammeh walifanya maandamano ya kutaka serikali imruhusu rais huyo wa zamani arejee nchini. Hata hivyo maafisa usalama walikabiliana vikali na waandamanaji hao.

Wakati yakijiri maandamano hayo, msemaji wa serikali ya Gambia alisema kuwa, serikali haiwezi kumdhaminia usalama Yahya Jammeh hauna iwapo atarejea nchini humo bila idhini yake.

Jammeh akiabiri ndege wakati akiondoka nchini Gambia

Yahya Jammeh, rais wa zamani wa Gambia, aliyelazimika kuachia madaraka na kukimbilia uhamishoni, hivi karibuni alivunja ukimya wake na kutangaza katika ujumbe wa sauti kuwa, ana mpango wa kurejea nyumbani.

Jammeh ambaye alitawala Gambia kwa mkono wa chuma kwa takribani miaka 22 alilazimika kuondoka nchini kwa udhalili baada ya maji kumfika shingoni, na hivi sasa anaishi uhamishoni nchini Equatorial Guinea.

 

Tags