Jan 27, 2020 14:59 UTC
  • Adama Barrow
    Adama Barrow

Polisi nchini Gambia imewatia mbaroni watu 137 na wengine zaidi ya 24 wamejeruhiwa baada ya maandamano yaliyokuwa yakimtaka Rais wa nchi hiyo, Adama Barrow atimize ahadi yake ya kuondoka madarakani baada ya kukalia kiti cha urais kwa miaka mitatu kubadilika na kuwa machafuko.

Barrow aliingia madarakani nchini Gambia katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 na hivyo kuhitimisha utawala wa miaka 22 wa Yahya Jammeh.

Rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh 

Hata hivyo Adama Barrow amekiuka ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi ya kuondoka madarakani mwezi huu akisema kuwa, katiba ya nchi hiyo inamtaka kuongoza nchi kwa muhula wa miaka mitano kamili. 

Ikijibu ukiukaji huo wa ahadi wa Rais wa Gambia, harakati ya "Three Years Jotna" yenye maana ya "Miaka Mitatu Inatosha" kwa lugha ya Wolof mwezi uliopita ilianza kufanya maandamano kumshinikiza Rais Barrow aondoke madarakani.

Jana Jumapili polisi ya Gambia waliingilia kati maandamano dhidi ya serikali katika mji mkuu Banjul huku na kutawanya waandamanaji walikuwa wakipiga nara kwamba wamepanga kumuondoa madarakani Rais Adama Barrow.

Msemaji wa serikali ya Gambia, Ebrima Sankareh amesema waandamanaji hao walifanya ghasia na vurugu kwa kuchoma matairi na magogo kwenye barabara kuu.

Sankrareh ameongeza kuwa, serikali imeamua kulipiga marufuku kundi la Three Years Jotna na kulitambua kuwa ni kundi la ghasia na maandamano haramu. Vilevile imevifungia vituo viwili vya redio ambavyo imesema vimechochea machafuko na ghasia wakati wa maandamano hayo. 

Tags

Maoni