Feb 03, 2020 06:55 UTC
  • Morocco yatangaza kuiunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya

Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imetoa tamko maalumu la kuitambua rasmi serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Shirika la habari la FARS jana lilinukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco ikitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Nasser Bourita, amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, Mohamed Taher Siala na kusisitiza kuwa nchi hizo mbili zina msimamo wa pamoja kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Libya.

Vile vile katika mtandao wake wa Twitter, Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imeandika kuwa, Rabbat inaiunga mkono kikamilifu serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kwani ndiye mwakilishi pekee wa nchi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ya Skhirat Morocco yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na aidha kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la umoja huo.

Jenerali muasi Khalifa Haftar katika mazungumzo na mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz

 

Makubaliano ya Shkhirat yalikuwa ya kisiasa na yalihusisha pande zote za Libya. Yalifikiwa mwaka 2015 kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Fayez al Sarraj, nayo imeundwa kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Hata hivyo jenerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono kikamilifu ya Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi kama vile Marekani na Ufaransa anakanyaga makubaliano hayo na tangu mwezi Aprili 2019 ameanzisha vita vikubwa vya silaha vya kutaka kuipindua serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa.

Tags

Maoni